Na. Nemes Michael, DODOMA
BARAZA la Madiwani
wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma limefanyika leo 29 Aprili, 2021 katika mkutano wake wa kawaida kupokea
na kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli kwa robo ya tatu ya mwaka
wa fedha 2020/2021 ya Halmashauri hiyo.
Mwenyekiti, Prof. Davis Mwamfupe |
Akifungua
mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, Mwenyekiti
wa baraza la hilo ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis
Mwamfupe aliwakaribisha wajumbe na viongozi wote huku akisema kuwa “karibuni katika
mkutano huu muhimu tujadili maslahi ya watu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
kama apendavyo Mwenyezi Mungu na siyo kama tupendavyo sisi” alisema Prof. Mwamfupe.
Wakichangia
masuala yanayohusu maendeleo ya sekta ya elimu ya msingi na sekondari katika
Jiji hilo, wajumbe wa Baraza hilo lenye Kata 41 na Madiwani 60, walisema kuwa uboreshwaji
wa elimu uwe kipaumbele katika Halmashauri Jiji la Dodoma.
Akijibu hoja za
wajumbe hao juu ya maendeleo ya elimu, Katibu wa mkutano huo, Wakili Msekeni
Mkufya alisema kuwa Halmashauri imeweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu
ya sekta ya elimu.
Katibu Wakili Msekeni Mkufya |
“Tunatumia
mbinu nyingi kuboresha sekta ya elimu hapa kwetu na kiujumla miundombinu ya elimu
ni kipaumbele kwetu. Hakuna siku tutafikia hatua kuwa tusahau madarasa, tusahau
madawati, sijui kama itawezekana sababu kwetu ni kipaumbele na Dodoma inakuwa kwa
kasi pia vitu vingi vinaendelea“ amesema Wakili Mkufya.
Lakini pia amemtaka
Mhandisi wa halmashauri kufanya tathmini ya hali ilivyo pamoja na mambo mengine.
Baada ya tathmini hiyo, utaratibu mwingine utafuata katika kutatua changamoto
za uboreshaji wa miundombinu ya elimu katika halmashauri hiyo, aliongeza.
MWISHO
Comments
Post a Comment