RAIS SAMIA ACHAGULIWA KWA KISHINDO UENYEKITI CCM TAIFA

Na. Jackline Kuwanda, DODOMA

Rais Samia Suluhu Hassan amechaguliwa kwa kishindo na Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa asilimia 100.

Mwenyekiti wa CCM (T), Samia Suluhu Hassan


Akitangaza matokeo hayo leo jijini Dodoma, Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema kuwa wajumbe waliopiga kura ni 1,862 na hakuna kura iliyoharibika wala kura ya hapana.

Idadi ya kura ni 1,862 hakuna kura iliyoharibika hata moja. Matokeo yake hakuna kura hata moja ya hapana, kura 1,862 ni sawa na asilimia 100’’ amesema Spika Ndugai.

Akizunguza mara baada ya kupata nafasi hiyo, Mama Samia amesema pamoja na ukongwe wa chama hicho na mafanikio yaliyopatikana zipo baadhi ya changamoto ambazo zinakikabili chama hicho, ikiwemo maslahi duni kwa watumishi wa chama.

Nafahamu kuwa kuna malimbikizo ya madai ya stahiki ikiwemo ya uhamisho na kustaafu, pamoja na hizo kuna changamoto kama hizo ufumbuzi wake ni kukaa kama chama kujitathmini  na tujirekebishe ili tuimarishe itikadi na imani yetu, natumia fursa hii kuwaahidi kuwa nitashirikiana na ninyi katika kuzitatua au kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo nilizo zitaja na nisizo zitaja’’ amesema Samia.

 

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM (T)

Awali, Mwenyekiti wa mkutano huo maalum, Philip Mangula ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, amesema lengo la Mkutano huo ilikuwa ni kufanya uchaguzi kutokana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Dkt. Magufuli kufariki dunia Machi 17, mwaka huu na hivyo, kwa mujibu wa Ibara 19 ya katiba inasema uongozi wa kiongozi utakoma iwapo kiongozi atafariki.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdulla Mabodi amesema pendekezo la kumchagua Mama Samia Suluhu Hassan limezingatia uwezo wake alio nao, upeo mkubwa katika masuala mbalilimbali ya uongozi kitaifa na kimataifa pamoja na siasa ya chama.

 “Ameyadhihirisha kwa vitendo kwa muda wote akiwa kiongozi mwandamizi ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ameonesha ukomavu, uwezo, weledi na umahiri mkubwa sana katika kipindi hiki ni muumini wa kweli kweli wa Mapinduzi, Muungano na Amani ndani ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania na Duniani kwa ujumla lakini pia ni mlezi wa demokrasia na mpenda maendeleo ya nchi yetu na watu wake,” Dkt. Mabodi.

Dkt. Mabodi amesema Kamati kuu ya Halmashauri Taifa CCM inaamini kwamba Mama Samia ni mtu sahihi anayeweza kuvaa viatu vilivyoachwa na Hayati Magufuli.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, amewataka watanzania kuugana na Rais Samia katika kutekeleza yote yaliyo mbele ambayo walianza pamoja Hayati Dkt. Magufuli.

Baada ya kifo cha Dkt. Magufuli kulitokea maswali na maneno mengi lakini kumbukeni maneno ya huyu mama akasema John Pombe Magufuli na mimi Samia Suluhu Hassan ni wale wale kwahiyo kama kuna watu mnaanza kujidanganya danganya, mnajidanganya wenyewe na mimi  naamini ndani ya chama hiki tuko imara,” amesema Pinda.

Akitoa salamu ya vyama vya siasa, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ahmed amesema wanamatarajio na Mwenyekiti huyo mpya na matumini yao kuwa atatoa ushirikiano mzuri kama ilivyokuwa kwa Hayati Magufuli.

Akimzungumzia Hayati Magufuli  na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Rodrick Mpogolo, amesema alileta mageuzi makubwa katika chama, kimuundo na kiuchumi na chama kuweza kuimarika kichumi hali inayopelekea sasa kujiendesha chenyewe.

Taifa limeondokewa na kiongozi mwenye maoni ambaye aliiwezesha Tanzaniakufikia uchumi wa kati, Hayati Dkt. Magufuli ameacha CCM imara na Serikali madhubuti, lakini idadi ya wajumbe waliohudhuria katika mkutanao huo ni 1,862 sawa na asilimia 99,” amesema Mpogolo.

 

MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.