Na. Veronica
Simba – TSC
Mwenyekiti wa
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba, ametoa hamasa kwa
watendaji wote wa Tume hiyo kusimamia vema suala la maadili kwa walimu ili
wajisikie fahari kuwahudumia.
Alitoa kauli
hiyo mwishoni mwa juma wakati akifunga mafunzo ya wajumbe wa kamati za wilaya
katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia ajira na maadili kwa walimu,
chini ya usimamizi wa TSC.
Akifafanua,
Prof. Komba aliwataka washiriki wa mafunzo husika, wanaporejea katika vituo
vyao vya kazi, kwenda kuwajibika kwa kuwakumbusha walimu maadili na miiko ya
kazi yao.
Alisema kuwa,
endapo Kamati hizo za Nidhamu zitafanikiwa kuwafikia walimu wote, TSC
itafanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya walimu wanaolalamikiwa kukiuka
maadili ya kazi yao.
“Sisi sote
tuone fahari ya kuwahudumia walimu wenye maadili ambayo watayaambukiza kwa
watoto wanaowafundisha na jamii kwa ujumla,” alisema.
Aidha,
Mwenyekiti huyo wa TSC aliwasisitiza washiriki wa mafunzo kujenga utaratibu wa
kujisomea sheria, kanuni, taratibu, miongozo na nyaraka za serikali kuhusu
masuala mbalimbali wanayoyashughulikia ili kujiongezea ufahamu wake.
Vilevile,
aliwataka wasisite kuomba ufafanuzi kutoka kwenye Ofisi au Mamlaka nyingine
hususan katika masuala yenye changamoto ili kuepuka kukosea katika utendaji wao.
Awali, akitoa
hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufunga mafunzo hayo, Katibu wa TSC, Mwl.
Paulina Nkwama alieleza kuwa lengo lilikuwa ni kuwawezesha washiriki kufahamu
na kutekeleza majukumu yao ya Tume kwa haki.
Mwl. Nkwama
alizitaja mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo kuwa ni pamoja na Kusudi la
kuanzishwa kwa Tume ya Utumishi wa Walimu, Muundo na Majukumu ya Tume pamoja na
Majukumu ya Tume kuhusu masuala ya Ajira na Maendeleo ya Walimu.
Aliongeza
kuwa, mada nyingine zilizowasilishwa ni kuhusu Maadili na Miiko ya Kazi ya
Ualimu pamoja na Majukumu ya Mamlaka za Nidhamu na Rufaa kwa Walimu.
Mafunzo hayo
ya siku mbili yalifanyika Aprili 28 na 29 mwaka huu jijini Mwanza na
kuzishirikisha wilaya zote za Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Mara, Kagera,
Simiyu na Shinyanga.
MWISHO
Comments
Post a Comment