PROF. KOMBA ATAKA TSC IONE FAHARI KUHUDUMIA WALIMU WENYE MAADILI

 

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba, akifunga mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia masuala ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu, Aprili 29, 2021 jijini Mwanza.

Na Veronica Simba – TSC

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Profesa Willy Komba, ametoa hamasa kwa watendaji wote wa Tume hiyo kusimamia vema suala la maadili kwa walimu ili wajisikie fahari kuwahudumia.

Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa juma wakati akifunga mafunzo ya wajumbe wa kamati za wilaya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia ajira na maadili kwa walimu, chini ya usimamizi wa TSC.

Akifafanua, Prof. Komba aliwataka washiriki wa mafunzo husika, wanaporejea katika vituo vyao vya kazi, kwenda kuwajibika kwa kuwakumbusha walimu maadili na miiko ya kazi yao.

Alisema kuwa, endapo Kamati hizo za Nidhamu zitafanikiwa kuwafikia walimu wote, TSC itafanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya walimu wanaolalamikiwa kukiuka maadili ya kazi yao.

“Sisi sote tuone fahari ya kuwahudumia walimu wenye maadili ambayo watayaambukiza kwa watoto wanaowafundisha na jamii kwa ujumla,” alisema.

Aidha, Mwenyekiti huyo wa TSC aliwasisitiza washiriki wa mafunzo kujenga utaratibu wa kujisomea sheria, kanuni, taratibu, miongozo na nyaraka za serikali kuhusu masuala mbalimbali wanayoyashughulikia ili kujiongezea ufahamu wake.

Vilevile, aliwataka wasisite kuomba ufafanuzi kutoka kwenye Ofisi au Mamlaka nyingine hususan katika masuala yenye changamoto ili kuepuka kukosea katika utendaji wao.

Awali, akitoa hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufunga mafunzo hayo, Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama alieleza kuwa lengo lilikuwa ni kuwawezesha washiriki kufahamu na kutekeleza majukumu yao ya Tume kwa haki.

Mwl. Nkwama alizitaja mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo kuwa ni pamoja na Kusudi la kuanzishwa kwa Tume ya Utumishi wa Walimu, Muundo na Majukumu ya Tume pamoja na Majukumu ya Tume kuhusu masuala ya Ajira na Maendeleo ya Walimu.

Aliongeza kuwa, mada nyingine zilizowasilishwa ni kuhusu Maadili na Miiko ya Kazi ya Ualimu pamoja na Majukumu ya Mamlaka za Nidhamu na Rufaa kwa Walimu.

Mafunzo hayo ya siku mbili yalifanyika Aprili 28 na 29 mwaka huu jijini Mwanza na kuzishirikisha wilaya zote za Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Shinyanga.

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.