Na. Jaqueline Kuwanda, DODOMA
Taasisi ya shirikisho la Vijana viongozi nchini,Youth Partnership
Countrywide [YPC] imeipongeza Serikali kwa kuendelea kufanyia maboresho sera ya
vijana ikiwemo Sera ya vijana ya namna ya kupata mikopo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika kongamano la vijana viongozi jijini Dodoma, Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya vijana ya [YPC] Israel Irunde amesema sera ya vijana kwa sasa inaruhusu kukopesha kuanzia vijana watano na si kumi kama ilivyokuwa awali.
"Tangu mwaka juzi na Mwaka jana tulizungumza sana kuwasaidia vijana
kwanini vijana wapewe mikopo wakiwa 10 wakati
hawafahamiani, kwanini watu wenye ulemavu walazimishwe kukaa kwenye kikundi cha
watu 10 wakati ni vigumu kuwakutanisha hata wawili lakini hivi karibuni, Waziri
Jafo wa TAMISEMI tayari alishatangaza kanuni zilishabadilishwa sasa vijana
wanaweza kupata mikopo hata wakiwa watano na watu wenye ulemavu anaweza kupata
mikopo serikalini hata akiwa mmoja" amesema.
Aidha, Mkurungenzi huyo wa YPC amesema ni wajibu kuwathamini
vijana pamoja na kuwepo wa maboresho ya sheria ya mahusiano kazini.
"Mara nyingi sana tumepigania kuhakikisha vijana wanapata kazi zenye staha
wakiwa wanaajiriwa au wamejiajiri wenyewe ,vijana wasitumiwe kama ndala, wajisikie nao wana maisha ya baadaye kuliko kukaa tu kwenye kazi ya
kukupatia chakula wakati mwingine chakula nacho shida, ili kila mmoja atoke kutoka kwenye eneo alilokuwa nalo hivyo hapa pana
hitaji maboresho zaidi sheria ya mahusiano kazini” amesema.
Fred Mtei ni Mratibu wa shiriki wa Kongamano la YPC amebainisha
lengo la kongamano hilo ni pamoja na namna ya kutatua changamoto za vijana huku
Irine Ringo akisema moja ya manufaa ya kongamano hilo ni kujiamini kwa
vijana.
Mwasilishaji wa Mada mbalimbali katika kongamano hilo la vijana la YPC, Adv. Dominick Nduguru mkurugenzi kutoka Taasisi ya Maendeleo ya vijana
ya Open Mind Tanzania amesema kuna uhitaji wa sera bora ya vijana pamoja na
watu wenye ulemavu kuhusishwa zaidi juu ya mapitio ya sera ya vijana.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kazi, Vijana, ajira na wenye ulemavu, Amina Sanga ametoa wito kwa vijana kuendelea kuchangamkia fursa
mbalimbali zinazotolewa na serikali kwa vijana ikiwemo mafunzo ya kujitolea ya
kuwajengea uwezo namna nzuri ya kuchangamana na watu mbalimbali ili kupata
fursa zinazoweza kujitokeza ikiwemo kubadilishana ujuzi na uzoefu.
"Vijana tunapaswa tuamke,tena ukisikia kuna warsha sehemu fulani
changamkia, changamoto ya vijana wa kileo akisikia kuna semina sehemu fulani ya
kumjengea uwezo lazima atauliza kuna posho, hajui kuna sehemu nyingine semina za
kujengewa uwezo mpaka ulipie lakini Tanzania tuna bahati nzuri sana unapewa
ujuzi lakini unataka ulipwe na ukisikia hakuna posho hauhudhurii, kumbuka
unapochangamana na watu mbalimbali hiyo ndiyo fursa na mwanzo wa maisha
yako hata siku moja wanaweza kukutafuta kuwa yule kijana ana mchango mzuri sana
tumchukue tu huyo" amesema.
Taasisi ya shirikisho la vijana ya YPC ilisajiliwa mwaka 2003 kama
kampuni isiyopata faida chini ya sharia ya makampuni na mwaka 2019 ilisajiriwa
kama asasi ya Kiraia [NGO] ikiwa na lengo wa kujenga uwezo kwa vijana jinsia zote ambapo
katika kongamano hilo vijana kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wamekutana
kujengewa uwezo ikiwa ni pamoja na namna ya vijana kufikia fursa.
MWISHO
Comments
Post a Comment