WAMILIKI WA MAABARA BUBU WAPEWA MWEZI MMOJA KUSAJILI MAABARA ZAO KUEPUKA KUFUNGIWA

 


Na Emmanuel Malegi – DSM

Wamiliki wa Maabara bubu nchini ambazo hazijasajiliwa wamepewa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo hadi Aprili 30 wawe wamesajili Maabara zao ili kuepuka kufungiwa.

Agizo hilo limetolewa mapema jana  na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe wakati wa mkutano na Wamiliki wa Maabara binafsi za Mkoa wa Dar Es Salaam wenye kauli mbiu isemayo “Ushirikiano wa Wadau ni nguzo Muhimu katika utoaji wa Huduma Bora za Afya” uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Mwalimu Nyerere mkoani humo.

Dkt. Grace amesema kumekua na ongezeko kubwa la Maabara bubu nchini ambazo nyingine zinafunguliwa katika makazi ya watu na kusababisha kuhatarisha Maisha ya watu wanaokaa maeneo hayo hususani Watoto ambao wana tabia ya kuchezea vitu hatarishi.

“Nimetoa maelekezo kwa mratibu wa Maabara Mkoa wa Dar Es Salaam kuhakikisha maabara zote ambazo hazijasajiliwa zipewe nafasi ya kusajiliwa hadi kufikia tarehe 30 mwezi Aprili, kinyume na hapo zitafungiwa na wahusika kuchukuliwa hatua kwa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria”. Amesema Dkt. Grace.

Dkt. Grace amesema huduma za Maabara ni huduma nyeti kwani zinahusika moja kwa moja na afya ya mwanadamu hivyo na endapo zitatoa majibu yasiyo sahihi zinaweza kuhatarisha Maisha ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa.

Aidha, Mkurugenzi huyo amesema kuna baadhi ya maabara ambazo hazina wataalamu wenye vigezo vinavyotakiwa au kuwa na upungufu kulingana na kazi zilizopo. Kutokana na hali hiyo, maabara hizo pia zimepewa mwezi mmoja hadi kufikia Aprili 30 wamiliki wa maabara hizo wawe wameshapata wataalamu wanaostahili kufanya kazi katika maabara hizo.

Pamoja na hayo, Dkt. Grace amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali za mitaa, vijiji na vitongoji kutoa taarifa kwenye mamlaka husika endapo wataona kuna maabara zimeanzishwa katika maeneo yao ambazo hazijasajiliwa na kulipa ada.

Nae Msajili wa Maabara binafsi Ndg. Dominic John amesema lengo la Mkutano huo ni kuwaleta wataalamu na wamiliki wa maabara wa Mkoa wa Dar Es Salaam ili waweze kupata miongozo na namna ya kuendesha maabara zao kwa usahihi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mwisho.

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.