Viongozi wa Dini Mkoani
Rukwa wakiongozwa na Kamati ya Amani Mkoani humo wameendesha dua maalum ya
kumuombea aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyeaga
dunia tarehe 17.3.2021.
Dua hiyo maalum
iliyofanyika katika viwanja vya Kumbukumbu ya Nelson Mandela Mjini Sumbawanga
ilihudhuriwa na wananchi mbalimbali wakiwemo, wazee maarufu, wazee wa kimila,
watumishi wa sekta mbalimbali Pamoja na wamachinga.
Awali, Kabla ya kuanza
kwa dua hiyo, Mwakilishi wa mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya
ya Kalambo Mh. Karolius Misungwi alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa na
serikali ya awamu ya tano chini ya aliyekuwa Rais wa awamu hiyo Hayati Dkt.
John Pombe Magufuli Pamoja na kumpongeza Rais wa awamu ya Sita Mh. Samia Suluhu
Hassan na kumtakia utekelezaji mwema wa majukumu yake.
“Nichukue Fursa hii kwa
niaba ya mkuu wa mkoa wetu kumpongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa
kuapishwa na kuwa rais wetu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyezi Mungu
amuongoze katika kuwatumikia watanzania wote bila ya kujali itikadi zao, bila
ya kujali rangi zao, na bila ya kujali makabila yao”.
“Sisi hatuna mashaka
kabisa na umahiri wa rais wetu mpendwa Mh. Samia Suluhu Hassan kwakuwa tunajua
kuwa atayaendeleza yote yale aliyoyaacha aliyekuwa mtangulizi wake, kazi
tuliyonayo sisi wanarukwa ni kumuombea na kumpa ushirikiano katika kulijenga
taifa letu,” Alisema.
Aidha, Mwenyekiti wa
Kamati hiyo ya Amani Baba Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya
Ziwa Tanganyika Rukwa na Katavi alieleza Ushujaa wa Hayati Dkt. John Pombe
Magufuli juu ya namna alivyoweza kupigania maslahi ya watanzania na hasa
wanyonge.
“sisi wanarukwa, kutoka
dini na madhehebu yetu yote,tumekutana mahali hapa katika umoja wetu, ili kwa
Pamoja tuutafute uso wa Mungu ili katika msiba huu Mungu Mwenyezi atujaalie
ustahimilivu akiachilia amani na mshikamano miongoni mwetu, tunamuomba Mungu
Taifa letu liwe na mshikamano, amani kati yetu watanzania itamalaki licha ya
msiba huu mkubwa wa kuondoka kwa aliyekuwa rais wetu wa awamu ya tano Dkt.
Magufuli,” Alielezea.
Kwa upande wake Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Rukwa Shekh Rashid Akilimali baada ya
kuelezea kazi nzuri iliyofanywa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alimuombea
Rais Mh. Samia Suluhu Hassan aweze kuvivaa viatu vilivyoachwa na hayati
magufuli ikiwa ni Pamoja na kuwashughulikia wezi na wala rushwa ndani ya
serikali.
“Tunamuombea avae viatu
hivyo, awe madhubuti na imara, akaze Kamba ile ile, madhalimu, majizi ndani ya
serikali, wala rushwa nidhamu maofisini irudi kama ilivyokuwa kwa Rais
Magufuli, tunaona nidhamu ilikuwepo, ulikuwa ukienda maofisini unaulizwa si
miaka ya nyuma na lile neno la pili unaniachaje halikuwepo tena, na walichukia
sana madhalimu na wezi ndani ya serikali,” Alisema.
Dua hiyo maalum
imefanyika ikiwa ni kuungana na watanzania wote nchini kumuombea aliyekuwa Rais
wa Taznania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ili Mwenyezimu Mungu ailaze roho
yake mahala pema peponi.
Comments
Post a Comment