Na. Albano Midelo, Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
PROGRAM
ya kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu (FORVAC katika Mkoa wa
Ruvuma inafanyakazi kwenye wilaya tano ambazo ni Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo
na Tunduru.
Mama Hilda Joseph mkazi wa kijiji cha Amanimakoro wilayani Mbinga akionesha aina mbalimbali za uyoga wa porini ambazo wanauza na kuongeza kipato |
Moja
ya maeneo ambayo FORVAC inatekeleza miradi yake ni katika Kata ya Amanimakoro
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambapo FORVACinawezesha mwananchi mmoja mmoja
na vikundi kuongeza thamani mazao ya misitu.
Mratibu
wa FORVAC Mkoa wa Ruvuma Marcel Mtunda anasema katika mwaka huu wa fedha
wanatarajia kutoa shilingi milioni 100 kwenye vikundi vya vijiji saba vilivyopo
kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Anasema
fedha hizo zitaviwezesha vikundi hivyo kutengeneza mizinga ya nyuki, vifaa vya
kulinia asali, vifaa vya kutengenezea vikapu na kuwawezesha akinamama
wanaookota uyoga kuwa na mitambo ya kuchakata uyoga ili uweze kupatikana hata
baada ya kipindi cha mvua.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Amanimakoro Ambrosi Nchimbi anasema kata yake
imebahatika kuwa miongoni mwa kata ambazo zipo kwenye mradi wa kuendeleza
mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu (FORVAC).
Anasema
katika kata yake kuna vijiji viwili vya Amanimakoro na Kiwumbi ambavyo
vinashiriki kwenye mradi huo ambapo vijiji vyote vinatekeleza mradi huo kwa
kutumia mlima wa Liyuni.
Aina mbalimbali za uyoga unaopatikana katika kijiji cha Amanimakoro wilayani Mbinga mkoani Ruvuma |
“Mipango
ya matumizi bora ya ardhi imeshafanyika katika vijiji husika,mafunzo ya Kamati
za Maliasili yamefanyika, lakini pia biashara ya mazao ya misitu imefanyika
ambapo kuna akina mama wameandaliwa kwa ajili ya mradi wa kukusanya uyoga
kwenye misitu” anasema Nchimbi.
Hata
hivyo anasema kabla ya mradi huo uyoga ukiwa porini ulikuwa unaoza na
kutotumika ipasavyo hivyo kupitia mradi huo wananchi watanufaika na uyoga kwa
kupata lishe na kuongeza kipato baada ya kuuza uyoga.
Nchimbi
anasema FORVAC imekusudia kusaidia mradi wa mashine za kukaushia uyoga ambao
utawezesha uyoga ukiwa mbichi uweze kukaushwa na kuhifadhiwa hatimaye kutumika
wakati wa kiangazi ambapo uyoga unakuwa haupatikani.
Kwa
mujibu wa Diwani huyo, katika kata yake kuna vikundi vya wafugaji wa nyuki
ambavyo vimeanza kuchonga mizinga na kuhifadhi kwenye misitu ili kufuga nyuki
na kupata asali hivyo kuinua uchumi wao.
Mmoja
wa wanufaika wa mradi wa uyoga katika kijiji cha Amanimakoro, Grace Hyera
anasema mradi wa kuokota uyoga unamwezesha kupata lishe na kuuza uyoga hivyo
kupata mahitaji mbalimbali ya familia.
Hata
hivyo anasema upatikanaji wa uyoga unategemea na eneo ambalo unakwenda kutafuta
kwenye msitu ambapo anasema kuna baadhi ya maeneo huota aina mbalimbali za
uyoga.
Diwani wa Kata ya Amanimakoro wilayani Mbinga Ambrosi Nchimbi akielezea namna wanawake katika kata yake wanavyofaidika na program ya kuongeza thamani mazao ya misitu |
Anazitaja
aina za uyoga unaopatikana katika eneo hilo kuwa ni ulelema, Ulundi, uinda,
ngaukau, ungala, unodo, kisanga, ukufu, mndyelesa, lukolombi na aina nyingine
nyingi za uyoga.
“Tangu
mdogo nilikuwa nakwenda na mama yangu porini ambaye alikuwa ananielekeza aina
zote za uyoga unaofaa kuliwa na uyoga ambao ni sumu’’, anasema Hyera.
Hata
hivyo anasema kwa siku moja anaweza kuokota uyoga na kujaza vikapu vitatu na
kwamba anapochemsha uyoga unapungua na anapoanika uyoga huo unapungua zaidi na
kupata kilo moja ambayo anauza shilingi 10,000.
Mary
Kapinga ni mmoja wa akinamama wanaookota uyoga katika kijiji cha
Amanimakoro,anazitaja baadhi ya changamoto ambazo wanakutana nazo kuwa ni kuharibika kwa uyoga inapotekea mvua
nyingi hali inayosababisha kukosekana jua la kutosha kukaushia uyoga.
Anasema
watakapopata mashine za kukaushia uyoga kama walivyoahidiwa na FORVAC utakuwa
ni msaada mkubwa katika kazi yao ya ujasirimali.
Kwa
upande wake Hilda Joseph anasema awali alikuwa hafahamu faida za uyoga licha ya
kutumia kama kitoweo hivyo anasema elimu waliopewa na FORAV kuhusu uchumaji
uyoga endelevu imewasaidia sana ambapo hivi sasa wanauza na kupata kipato.
“Kupitia
uyoga tunapata pesa ambazo zinawapeleka watoto shuleni, tunapata pesa za
kukidhi mahitaji mbalimbali kama chakula na kununua pembejeo za kilimo’’, anasema.
Hata hivyo anatoa rai kwa FORVAC kuwapatia mbegu ambazo zitawawezesha kupanda uyoga majira ya kiangazi ili muda wote wawe na soko la uyoga.
Mama Hilda Joseph mkazi wa kijiji cha Amanimakoro wilayani Mbinga akionesha aina mbalimbali za uyoga wa porini ambazo wanauza na kuongeza kipato |
Akizungumzia
changamoto ya nyoka kwenye uyoga,Hilda anasema nyoka anapenda sana kula uyoga
ambapo huwa anajiviriga kwenye uyoga mkubwa na kwamba wakati fulani inawalazimu
kukimbia na kuacha uyoga kwa sababu nyoka chakula chake kikuu ni uyoga.
Anasema
wanaanza kuchuma uyoga kuanzia Desemba hadi Aprili kila mwaka ambapo anasema
uyoga wa kuliwa unajulikana na uyoga wa sumu pia unajulikana.
Anazitaja
sifa za uyoga unaoliwa kuwa ni uwepo wa wadudu,unanukia na nyoka wanapenda uyoga wa aina hiyo
ukilinganisha na uyoga wenye sumu.
Jackson
Boimanda ni Mshauri wa Biashara wa FORVAC Halmashauri ya Mbinga anasema mafunzo
ambayo hadi sasa wameyatoa kwa akinamama hao yamewasaidia kuwajengea uwezo
katika biashara ya uyoga.
Anasema
FORVAC tayari imeandaa bajeti ya kuwanunuliwa akinamama hao vitendeakazi
ikiwemo mabuti,epuloni,mashine za kukausha uyoga na vifaa vingine walivyoviomba
ili waweze kufanyakazi ya kuokota uyoga kwa ufanisi na tija.
Baadhi ya wanawake katika kijiji cha Amanimakoro wilayani Mbinga wakiwa kwenye msitu wanafanyakazi ya kuokota uyoga kwa ajili ya lishe na kuongeza kipato |
“Moja
ya majukumu yangu ni kuwaunganisha akinamama hawa na masoko,hivyo tunawatafutia
masoko ili waweze kuuza kile wanachokizalisha,kuna Taasisi ambazo zipo tayari
kutoa mafunzo na kununua uyoga wakiwemo WWF ambao wanahitaji tani nyingi za
uyoga’’, anasema.
Naye
Mwenyekiti wa kijiji cha Amanimakoro Moses Nyoni anasema wananchi wanapata
faida kubwa kutokana na mradi wa FORVAC ikiwemo kupata lishe na kipato.
Anaishauri
FORVAC kuongeza bajeti katika program ya kuongeza thamani mazao ya misitu ili
wananchi wengi waweze kunufaika kupitia mradi huo.
Comments
Post a Comment