Waziri Mkuu aziaagiza Mamlaka za serikali za mitaa kutenga bajeti za kuhifadhi maeneo ya kihistoria

Na. Albano Midelo, Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma

WAZIRI Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameiagiza mikoa na Mamlaka zote za serikali za mitaa kutenga bajeti ya kuyahifadhi maeneo yote ya kihistoria ili kutopoteza historia yake kwa manufaa ya Taifa.

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Innocent Bashingwa ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu katika tamasha la miaka 114 ya mashujaa wa vita ya Majimaji 


Majaliwa ametoa agizo hilo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa kwenye kilele cha tamasha la kumbukizi ya miaka 114 ya vita ya Majimaji lililofanyika kwenye viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea.

Waziri Mkuu pia ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kuadhimisha kumbukizi hizo ili ziwe sehemu ya vivutio vya utalii nchini ambazo zinachangia kuongeza pato la Taifa na kwamba Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Habari zihamasishe na kuelimisha jamii fursa za kumiliki maeneo ya malikale.

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo InnocentBashungwa akiweka ngao kwenye mnara wa mashujaa wa vita vya Majimaji ambapo mashujaa 67 walinyongwa na wajerumani mwaka 19069


Akizungumzia mashujaa wa vita ya Majimaji, Waziri Mkuu ameagiza kumbukumbu zilizopo ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji zinaendelea kuhifadhiwa ili kujenga uzalendo na kuleta utaifa kwa kizazi kilichopo na kijacho.

“Mkoa wa Ruvuma hivi sasa una makumbusho mawili ambayo ni Makumbusho ya Majimaji na Makumbusho ya Dkt. Hayati Rashid Mfaume Kawawa,Mkoa huu ndiyo kitovu cha kusaidia wanaharakati wa ukombozi wa Afrika hususan nchi jirani ya Msumbiji’’,alisisitiza Waziri Mkuu.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Songea mjini, Dkt. Damas Ndumbaro  akizungumzia kumbukizi ya miaka 114 tangu kunyongwa mashujaa wa vita Majimaji,amesema maadhimisho hayo yamelenga kuenzi ushujaa  wa wazee wetu katika harakati za awali za ukombozi dhidi ya wakoloni.

Imanuel Zulu Chifu wa Tano wa kabila la wangoni akizungumza kwenye kumbuzi ya miaka 114 ya vita ya Majimaji


“Maisha ya wazee wetu ni fahari yetu kwa sababu wazee hawa walipigania nchi kwa uzalendo wa hali ya juu,ukombozi wa mwafrika una historia kubwa sana hapa kwa sababu mapambano yaliyofanyika kwa muda mrefu zaidi dhidi ya mkoloni nchini Tanzania yalifanyika Songea’’, alisema Dkt. Ndumbaro.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Christawaja Ntandu ameyataja malengo ya tamasha la kumbukizi ya mashujaa wa majimaji ambalo hufanyika kila mwaka kuwa ni  kukumbuka na kuwaenzi mababu zetu ambao walinyongwa Februari 27,1906 na kuzikwa kwenye makaburi mawili ndani ya makumbusho ya Majimaji.

Hata hivyo amesema tamasha hilo hutoa fursa kwa wananchi kutunza,kuenzi na kuendeleza uzalendo,amani na mshikamo ambao umerithiwa kutoka kwa mababu zetu na kwamba tamasha hilo pi hutumika kuibua na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo ukanda wa kusini.



Naye Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga amesema wazee waliopigana katika vita ya Majimaji miaka 114 iliyopita dhidi ya wakoloni walitoa mchango mkubwa katika kutetea taifa letu na kwamba vita ya Majimaji imebeba utajiri mkubwa wa historia ya ukombozi na uhuru wa nchi yetu.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.