Na. Zuena Msuya Simiyu
Naibu Waziri Wa Nishati, Wakili Stephen
Byabato ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufanya vikao vya mara kwa
mara na wafanyakazi wa shirika hilo kwa kila Kitengo na Idara husika ili
kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi hao.
![]() |
Naibu Waziri Wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Simiyu, wakati wa ziara yake mkoani humo, Februari 25, 2021 |
Wakili Byabato alisema hayo, wakati akizungumza
na wafanyakazi wa shirika hilo mkoani Simiyu Februari 25, 2021, wakati wa ziara
yake mkoani humo.
Alisema vikao hivyo vihusishe
wafanyakazi wote bila kujali viwango vya elimu na ngazi za madaraja walizonazo,
ili kila mtumishi aweze kueleza yanayomsibu sehemu za kazi pamoja na kueleza
namna bora ya kuboresha utendaji kazi wao.
Aliwaeleza kwamba vikao hivyo ndivyo
vinavyowafanya wafanyakazi kujiona wao ni sehemu ya familia ya shirika kwa kuwa
wanapata muda wa kukaa pamoja na kuzungumza na viongozi wao.
Aidha alitaka watumishi hao kupewa
nafasi ya kutoa maoni au mapendekezo yao ya nini kifanyike ili kuboresha
utendaji kazi wao pamoja na shirika kwa jumla na maoni hayo yasikilizwe na
kufanyiwa kazi.
“Mfanyakazi hutumia muda mwingi wa
maisha yake sehemu ya kazi, eneo hili ni muhimu sana kwa kuwa wote hujiona ni
familia moja licha ya kila mmoja kutekeleza majukumu yake, hivyo ni muhimu
viongozi wa eneo husika kuweka utaratibu kuwa na vikao vya pamoja ili waweze
kueleza changamoto zao, na zifanyiwe kazi kwa wakati sahihi, hii inaongeza
morali ya kufanya kazi muda wote kwa kasi, ubunifu na usahihi, na katika vikao
hivyo mara nyingi hupatikana mawazo chanya ya kujenga na kuimarisha zaidi ubora
wa shirika”, alisema Wakili Byabato.
Katika hatua nyingine aliwaonya
watumishi hao kufika kazini wakiwa wamelewa ama kunya pombe muda wa kazi, na
atakayebainika kuwa na tabia hiyo achukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa
sheria za kazi.
Hata hivyo alipongeza wafanyakazi wa
shirika hilo mkoani humo kuwa wamekuwa wakifanya kazi zao kwa umakini na kutoa
huduma nzuri kwa wateja licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili za
kukatika umeme mara kwa mara mkoani humo.
Aidha aliwaeleza kuwa waendelee kuwa
wavumilivu kwakuwa muda si mrefu
changamoto hiyo itatuliwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha kupoza
umeme cha Imalilo.
Kituo hicho kitakuwa na uwezo kuzalisha
umeme wa Megawati 90 itakayokuwa ikitumika katika mkoa huo na mikoa jirani,
mahitaji ya umeme kwa Simiyu kwa sasa ni Megawati 10 tu.
Mkoa wa Simiyu unapokea umeme kutoka
mkoani shinyanga na hivyo kuufanya umeme huo kuwa na nguvu ndogo kuhimili
matumizi halisi.
Comments
Post a Comment