Naibu waziri wa Nishati asisitiza kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na usahihi

Na. zuena msuya MARA

 

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, ametaka wafanyakazi wa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na usahihi kwa maslahi mapana ya nchi na taifa kwa jumla.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato(katikati), akipata maelezo jinsi Kituo cha Kupoza Umeme cha Mkoa wa Mara kinavyofanya kazi, alipotembelea kituo hicho, wakati wa ziara yake mkoani humo


Wakili Byabato alisema hayo wakati wa ziara yake mkoani Mara, Februari 26,2021, ambapo alizungumza na wafanyakazi wa (TANESCO) pamoja na kutembelea Kituo cha Kupoza Umeme cha  mkoa huo kinachozalisha Megawati 24, matumizi halisi kwa sasa yakiwa ni megawati kumi nukta saba (10.7).

Alisema kuwa kwa kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na usahihi kutawezesha shirika hilo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwahudumia watanzania wote kwa wakati sahihi.

“Wafanyakazi wa TANESCO wanadhamana kubwa ya kuhakikisha kuwa umeme unasambaa Tanzania nzima kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, ni wakati sahihi kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na usahihi ili kutimiza azma ya serikali ya kufikisha umeme kwa watanzania wote na kukuza uchumi wa viwanda”, alisema Wakili Byabato.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (kushoto) akiteta jambo na kaimu meneja wa shirika la umeme tanzania (TANESCO) Mhandisi Hamis Kadoma (kushoto) wakati wa mkutano wake wafanyakazi wa Shirika hilo mkoani humo 


Akizungumzia kituo cha kupoza umeme cha mkoa wa Mara, alisema kuwa kituo hicho kilizinduliwa mwaka 1989 na kinapokea umeme kutoka katika maeneo manne (Fider) ambayo ni katikati ya mji wenye wa Mara, Butiama, Tarime na Majita.

Aidha alisema kuwa, hivi karibuni serikali inatarajia kutanua   kituo hicho ili kongeza uwezo wake wa kuzalisha umeme.

Vilevile aliwataka wawekezaji kuwekeza katika mkoa huo kwa kuwa kuna umeme mwingi na wa kutosha.

Baadhi ya Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), mkoani Mara wakimsikiliza, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, (hayupo pichani) wakati wa mkutano wake na wafanyakazi hao alipofanya ziara mkoani humo


Katika hatua nyingine aliwataka watanzania kulinda miundombinu ya umeme iliyopita na kusambazwa katika maeno yao.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.