NAIBU WAZIRI ATOA ONYO KWA MENEJA WA RUWASA CHATO

Na. Fatuma Malende, CHATO

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ametoa onyo kwa Meneja wa Wakala wa MajiSafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Chato, Mhandisi Andrew Kilembe kwa kushindwa kutatua kwa wakati kero ya ubovu wa mita za maji zilizowekwa katika mradi wa maji wa Imalabupina Inchwankima na kusababisha wananchi wa eneo hilo kukosa maji kwa siku kadhaa.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) akikagua miundombinu ya mradi wa maji wa Imalabupina Inchwankima


Ametoa onyo hilo baada ya kupokea malalamiko toka kwa wananchi wakati akikagua mradi huo unahohudumia wakazi wa vijiji hivyo.

Amesema wananchi wanakosa huduma ya maji kwa sababu ya viongozi kufanya kazi kwa mazoea na kushindwa kutatua kero zinazojitokeza kwa wakati.

“Natoa onyo na naomba fuatilieni hilo tatizo linalosababisha wananchi wasipate maji kwa wakati maeneo mengine yanatoa maji, na hakikisheni hizo mita zinazosumbua zinabadilishwa haraka ili kuondoa kero hiyo na wananchi hawa wapate maji”, amesema Mhandisi Mahundi na kusisitiza kezo zote ikiwemo matatizo ya umeme yasisubiri viongozi.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) akiwa ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Chato, Eng. Charles Francis Kabeho kabla ya kuanza ziara ya kukagua miradi ya maji katika Wilaya ya Chato


Aidha, amempongeza Meneja huyo wa RUWASA Chato kwa kuamua kutumia shilingi milioni 311 kukarabati miundombinu ya mradi wa maji Kasenga ambao ulichakaa na kuacha kutoa maji kwa muda mrefu.

Katika ziara yake ya kukagua miradi ya maji mkoani Geita Naibu Waziri alikagua pia mradi wa maji wa Katoro Buseresere ambao utekelezaji wake unaendele vizuri na mradi huo ukikamilika utahudumia wananchi 20,000 wa kata ya Buseresere, Katoro, Ludete na Nyamigota.

Tenki la maji la mradi wa maji Katoro ambalo ujenzi wake unaendelea viruzi linasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA).


Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.