Na. Fatuma Malende, GEITA
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi MaryPrisca
Mahundi (Mb) amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa
Mazingira Geita Mhandisi Frank Changawa kuhakikisha mkandarasi wa awali aliyekuwa
anatekeleza mradi wa Nyamtukuza Petty and Company (Ltd), kurejesha pampu ya
mradi huo aliyorudishiwa kwa ajili ya matengenezo madogo ili iweze kufungwa na
wananchi waendee kupata huduma ya majisafi na salama.
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) akifungua maji katika bomba kuashiria kukamilika kwa mradi wa maji katika Kata ya Kalumwa iliyopo katika Wilaya ya Nang’hwale mkoani Geita |
Ametoa kauli hiyo alipokuwa anakagua utekelezaji
wa mradi huo ambao umechukua muda mrefu kukamilika kutokana na wakandarasi kushindwa
kukamilisha mradi kwa wakati hadi mkataba ulipovunjwa na kazi ya utekelezaji
kuchukuliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA).
“Ninawapa siku saba (GEUWASA) kuhakikisha pampu iliyochukuliwa
na Mkandarasi kwa ajili ya matengenezo inarejeshwa haraka ili ije ifungwe kwenye
mradi kama mchoro wa awali unavyoonesha kufunga pampu mbili ili moja ikipata
hitilafu, basi nyingine iendelee kufanya kazi, wananchi waendelee kupata huduma
ya maji”, amesema Mhandisi Mahundi, na kusisitiza kuwa ndani ya siku hizo saba
kupatiwa ripoti ya pampu hiyo kama imerejeshwa.
Amesema wananchi wengi nchini hususani wa maeneo
ya vijijini wanahitaji maji na hivyo
kuwataka watekelezaji wa miradi hiyo kukamilisha kwa wakati unaotakiwa ili
wananchi wapate huduma wanayostahiki.
Aidha, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka
ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA) na watendaji wake kwa kuweza
kutekeleza mradi huu ambao hapo awali ulikuwa kati ya miradi kichefuchefu kwa
kutokamilika kwa wakati na sasa mradi umefikia hatua za mwisho na baadhi ya
wananchi wa Nyamtukuza wameanza kupata huduma ya majisafi. salama na yenye
kutosheleza.
Mradi wa Nyamtukuza kwa sasa unatekelezwa na
GEUWASA kwa kutumia wataalam wa ndani (Force
Account) na umegharimu shilingi bilioni 11 ambapo kwa kutumia watalaam hao
wa ndani serikali imeweza kuokoa shilingi bilioni 4 na unatarajiwa kukamilika
mwishoni mwa mwezi machi, 2021.
Comments
Post a Comment