NA DOTTO
KWILASA,DODOMA.
Matokeo ya Utafiti wa mbegu kwa wakulima unavyoibua zao la Ndizi Dodoma.
WAKATI nasoma shule ya msingi,moja ya mambo niliyofundishwa ni kuhusu mazao yanayopatikana Tanzania na asili ya mazao hayo kwa kila mkoa.
Namkumbuka sana
mwalimu wangu wa somo la Jiografia alinifundisha kuwa nchini hapa kilimo cha
Mpunga kinalimwa zaidi Kyela,Mahindi-Iringa,Karanga-Kongwa,Miwa-Kirombero
,Ndizi -Bukoba wakati Korosho ikilimwa zaidi Mtwara.
Na huu ndiyo
ulikuwa mfumo wa kilimo kabla kuanza mapinduzi ya ukuaji wa sekta ya
kilimo cha kisasa sambamba na matumizi ya teknolojia bora zikiwemo mbegu bora
za kilimo.
Mazoea haya
yalidumaza sana suala la kilimo kwani iliwabidi wakulima kulima mazao
yaliyozoeleka katika eneo husika huku sababu ya kufanya hivyo ikitajwa kuwa ni
kila mmea hustawi kulingana na hali ya hewa ya eneo husika.
Hali hiyo
inabadilika sasa,kadri siku zinavyokwenda mambo yanabadilika ,unaweza kusema
kuwa watu wanaenda na wakati .
Namaanisha kuwa
kulima kwa mazoea kumepitwa na wakati unaweza ukawa Shinyanga na ukakuta
wakulima wa huko wanalima mazao yaliyozoeleka kulimwa Dodoma hali inayopunguza
uhaba wa chakula kwa kiasi kikubwa.
Hatua hii
imetokana na faida ya uwepo wa Wataalam wa utafiti wa mbegu bora za kilimo
ambao hutumia muda mwingi kubuni mbinu za kuzalisha mbegu za kisasa ili
kumrahisishia mkulima kulima kwa faida na kuondoa umaskini .
Hii imejidhihirisha mkoani Dodoma ambako kwa kiasi kikubwa sasa wakulima wanaanza kuhamasika na kilimo cha mazao ya kimkakati Kama vile Ndizi,korosho na Mpunga kwa maeneo ya Wilaya Bahi na kitongozu cha Swaswa nje kidgo ya Jiji la Dodoma jambo ambalo mwanzo halikuwepo .
kiuhalisia hali ya hewa katika mkoa huu ni savana kavu ambayo huwa na kipindi kirefu cha ukame kuanzia mwezi Aprili hadi mwezi Desemba, na kipindi kifupi cha mvua katika miezi inayosalia.
Aidha wastani wa
mvua katika mkoa huu ni milimita 570 na asilimia 85 ya wastani huu
hunyesha kwa miezi minne yaani kati ya mwezi Desemba na mwezi Machi kila mwaka.
Licha ya kuwa
imezoeleka maskioni mwa wengi kuwa Dodoma ni kame,kauli hii hupingwa na wanamazingira
wengi huku wakisistiza kuwa mkoa huu una asili ya maji mengi kuweza kusapoti
kilimo cha umwagiliaji ikiwa jamii itakubali kubadili mtizamo huo.
Kutokana na hayo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Samia Suluhu Hasan katika uzinduzi wa kampeni yake ya
kujanikisha Dodoma iliyofanyika Desemba 21 mwaka 2017 katika
eneo la Mzakwe Kata ya Makutupora Manispaa ya Dodoma alizitaka Halmashauri za
Mkoa wa Dodoma kutunga Sheria Ndogo zitakazomtaka kila Mkazi wa eneo katika
Mkoa huo kupanda miti ili kupambana na mabadiliko ya hali tabia Nchi.
Alisema upandaji miti si kwa ajili ya
kuhifadhi mazingira tu bali ni fursa ya kilimo, kukabiliana na mabadiliko ya
tabia nchi ambapo alitolea mfano mti mmoja uliokomaa unaweza kunyonya kiasi cha
kilogramu 150 za gesi ya hewa ya ukaa kwa mwaka na hivyo kusaidia kupunguza
joto kwenye uso wa dunia, na pia kusaidia kuboresha afya ya mwili na akili.
Hali hiyo
imesaidia kwa kiasi kikubwa ambapo sasa utafiti wa mbegu bora za
mtama,zabibu,migomba,alizeti,mihogo na uwele zinaendelea kuwanufaisha wakulima
katika mkoa huu na kupata mazao mengi yenye ubora wa viwango vya kisayansi.
Ili kutoa nafasi kwa wakulima wengi
zaidi kujifunza kuhusu uzalishaji wa ndizi ,Mtafiti wa Idara ya Udongo kituo
cha utafiti TARI-Makutupora Ashura Ally anasema,Kawaida
migomba inaweza kupandwa kwa utaratibu
wa nafasi ya umbali wa mita 2.75 kwa
2.75, kigezo hiki mara nyingi kinakuwa kwa migomba mifupi na umbali wa
mita 3 kwa 3, kwa migomba ya urefu wa kati huku umbali wa mita 3.6 kwa 3.6, kwa
migomba mirefu zaidi
Anazidi kueleza kuwa uchimbaji mashimo
inafaa ufanywe mapema kabla ya muda wa kupanda Shimo lichimbwe kwa kutenganisha
udongo wa juu na wa chini.
“Iwapo utachimba shimo la mviringo
litafaa liwe na kipenyo cha sentimeta 60 hadi 90 na kina cha sentimeta 60 hadi
90,iwapo utachimba shimo la mstatili au mraba litakuwa na urefu, upana na kina
cha sentimeta 60 hadi 90, kutegemea kiasi cha mbolea kilichopo na kiasi cha
kvua kinachonyesha sehemu hiyo,”anasema.
Pamoja na mambo mengine anaeleza
uwekaji wa mbolea hufuata mara baada ya mashimo kuwa tayari Mbolea ya samadi
iliyooza vizuri au mboji iwekwe kwenye lundo la udongo wa juu kando ya kila
shimo na tayari kusubiri kuja kurudishiwa kwenyeshimo baada ya mche/machipukizi
kuwekwa kwenye shimo.
“Zao la ndizi
huweza kuanza kuvunwa katika kipindi cha miezi 9 hadi miezi 15 tangu kupandwa
,Muda wa kuvunwa hutegemea hali ya hewa ambapo sehemu za joto ndizi huvunwa
mapema zaidi kuliko sehemu za baridi,Pia migomba iliyopandwa kwa kutumia
machipukizi huzaa mapema kuliko iliyopandwa miche iliyozalishwa kwa chupa
(tissue culture),”anafafanua.
Dosca David ni mmoja wa wakulima
mkoani hapa ambaye ametumia fursa ya uwepo wa vituo vya utafiti wa mazao na
kuanza kulima zao la ndizi jambo linalowashangaza wengi.
"Wengi walinishangaa ,hawajazoea
kuona mashamba ya Migomba Dodoma,wengi walinibeza lakini kwa kuwa nilijiamini
na kuamini elimu niliyopewa na Watafiti sikuwa na shaka,"alisema kwa
kujiamini.
Anasema pamoja na kuwa ni zao la
kibiashara kwa soko la ndani bado njia bora zikitumika katika kuzalisha migomba
inayotoa ndizi zinazokidhi vigezo vya uhitaji wa soko la nje itasaidia zaidi
kukuza vipato vya wakulima mkoani Dodoma.
“Niliamua kutafuta eneo linalofaa kwa
kilimo katika Kijiji cha Mtumba(mji wa Serikali) eneo ambalo lipo kimkakati
zaidi hasa Kutokana na Ofisi nyingi za Serikali kuwepo mahali hapo,
Jambo hili limewavutia wenyeji wengi
wa Kijiji hiki na kuanza kuiga,naweza kusema nimekua mfano wa kuigwa ,ukifika
Mtumba karibu kila nyumba ina Migomba japo si mingi lakini inatia moyo
kwamba utaalamu wa utafiti wa mazao unafanya kazi,"anaeleza.
Hata hivyo anasema kabla ya kuanza
kilimo hicho alitafuta ushauri wa kitaalam katika kituo cha utafiti
TARI-Makutupora ambapo alishauriwa kuwa zao hilo linafaa kulimwa kutokana na
hali ya hewa Kiasi cha chini cha mvua kifaacho ni 100mm kwa mwezi au
1200mm kwa mwaka,
“Mtafiti wa Idara ya Udongo kituo cha
utafiti TARI-Makutupora alinipa maelekezo ya kuanzia
uandaaji wa mashamba hadi kufikia uvunaji wa zao hilo jambo linalotia moyo
zaidi ni kuwa wakati wowote mimi na wakulima wenzangu tunapohitaji ushauri
tunapewa elimu bure,”anafafanua.
“Alinieleza Mgomba hustawi zaidi
kwenye Udongo wenye rutuba ya kutosha,Usiotuamisha maji na usio na chumvi,
Chachu ya udongo inafaa iwe kati ya pH
5 mpaka pH 8 ndicho nilichofanya,”anafafanua.
David anaeleza kuwa Migomba huhitaji
maji mengi hivyo kutokana na hali ya hewa ya mkoa huo humlazimu Wakati wa
kiangazi kutumia zaidi kilimo cha umwagiliaji kuepuka kudhoofisha mimea yake.
"Baada ya kujifunza vizuri kuhusu
zao hilo nilichukua jukumu la kuandaa sehemu husika ambapo kwa kuanza alianza
kilimo cha majaribio katika eneo lenye ekari Moja wazo ambalo limezaa matunda
,"anasema
Hata hivyo anatumia nafasi hii kuwatoa
hofu wakulima wanao ogopa kulima mazao mengine na kusema kuwa wanapaswa kutumia
fursa ya Dodoma kuwa makao makuu na kuanza kuwatumia wataalamu wa utafiti wa
mazao kuwasaidia mbegu bora na kujikita zaidi katika kilimo cha
umwagiliaji kuondokana na uhaba wa chakula.
Mbali na hayo ameiomba Serikali
kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuendelea kusambaza
matokeo ya Utafiti wa mbegu kwa wakulima ili kuongeza tija.
Mwishooo.
Comments
Post a Comment