RC Mndeme aagiza watendaji kusimamia utunzaji vyanzo vya Maji

Na. Albano Midelo, Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma

 

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewaagiza maafisa Tarafa na viongozi wote ngazi ya Wilaya kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji ili viwe endelevu.

Aliyesimama ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akiongoza kikao cha wadau wa maji mkoani Ruvuma

Mndeme ametoa agizo hilo wakati anafungua mkutano wa wadau wa sekta ya maji mkoani Ruvuma kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.

Mndeme pia ameagiza wote wanaofanya shughuli za kiuchumi kwenye vyanzo vya maji kuondolewa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 ya sheria ya RUWASA ya mwaka 2019.

Maagizo mengine yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa katika kikao hicho ni Halmashauri zote na sekretarieti ya Mkoa kuwajibika kikamilifu katika kutekeleza na kusimamia majukumu yote yaliyoorodheshwa kwenye sheria namba tano ya huduma ya maji ya mwaka 2019.

“Mameneja wa RUWASA Wilaya kwa kushirikiana na Halmashauri zote zihakikishe kwamba miradi iliyopo na mingine itakayojengwa inaunda vyombo huru vya watumiaji maji kwa sheria namba tano ya mwaka 2019 kabla au ifikapo Mei 31,2021’’,alisisitiza Mndeme.

Mndeme pia ameagiza katika kikao cha Baraza la madiwani cha kila robo katika Halmashauri zote iwepo mada ya kudumu ambapo Mameneja wa RUWASA katika wilaya husika watatoa taarifa kuhusu hali ya upatikanaji na usajili wa vyombo vya watumiaji maji.

Mkuu wa Mkoa pia ameagiza  RUWASA Wilaya na Mkoa  zishirikiane na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa mazingira SOUWASA sanjari na ofisi za mabonde ya maji katika kutafuta vyanzo vya maji na kuandaa mipango ya utunzaji wa vyanzo vya maji.

Baadhi ya wadau wa maji mkoani Ruvuma wakifuatilia kikao cha kilichofanyika ukumbi wa Manispaa ya Songea kikiongozwa na Mkuu na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma 


“Naagiza fedha zitokanazo na mauzo ya maji zikaguliwe na mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ili kujiridhisha namna fedha hizo zilivyotumika,endeleeni kuwachukulia hatua wanaoharibu kwa makusudi miundombinu ya maji na vyanzo vya maji’’,alisema Mndeme.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga ameyataja majukumu ya RUWASA kuwa ni kuandaa mipango ya kusanifu miradi,kujenga na kusimamia uendeshaji wake.

Majukumu mengine ni kuendeleza vyanzo vya maji kwa kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi,kuchimba visima na kujenga mabwawa sanjari na kufanya matengenezo makubwa ya miundombinu ya maji.

 

MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.