Netho Sichali, Afisa habari Wilaya ya Nyasa
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala
Bora, Dr Laurean Ndumbaro amewataka watumishi wa Umma Nchini, kutoa Huduma Bora,
na kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili ili wapate
maendeleo.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki hii, alipokuwa
akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Nyasa katika Ukumbi wa Kapten John Komba,
alipofanya Ziara ya Kikazi Wilayani
Nyasa yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za watumishi Wilayani
hapa.
Dkt Ndumbaro amefafanua kuwa, Serikali ya awamu ya Tano
inawategemea sana watumishi wa Umma, katika kila eneo la utoaji Huduma, ili
waweze kutoa huduma bora kwa wananchi ambao kodi zao ndizo zinawalipa
mishahara, hivyo wana kila sababu ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapewa huduma
bora ili waipende Serikali yao.
Amewaagiza watumishi wa Umma kutoa huduma bora kwa
kila mtumishi kutokana na Taaluma yake kwa wakati, kwa lengo la kuwajibika na kutatua
kero za wananchi ili wananchi waweze kupata maendeleo.
“Napenda kuwakumbusha sisi ni Watumishi wa Umma, hivyo
tuna kila sababu ya kuwapenda wananchi na kuwatumikia, na yeyote anayehitaji
huduma katika Ofisi za Umma, apate huduma bora, na kila Mtumishi atoe Huduma,
kulingana na Taaluma yake kwa kuwa wananchi hawa kodi zao wanazolipa, ndizo
zinatulipa Mishahara. Aidha serikali ya awamu ya Tano imedhamiria Kutoa Huduma
Bora kwa Wananchi hivyo kila Mtumishi wa Umma ajione analazimika kuwahudumia
wananchi, na tunatakiwa kufahamu, sisi sio wafanyakazi wa Umma bali ni
Watumishi wa Umma”.
Alisema, na kuwataka wakuu wa Idara na Vitengo kuwahudumia
watumishi wanaofika kupata huduma katika Ofisi zao kwa haraka ili nao wakatoe
huduma katika Sehemu zao za kazi kwa kuwahudumioa wananchi ipasavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Nyasa Bw Jimson Mhagama amempongeza Katibu Mkuu wa huyo kwa kufanya Ziara
katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa na kumuahidi yote aliyoyaagiza kama Mkuu
wa Taasisi, atasimamia na kuhakikisha Watumishi wanawajibika ipasavyo ili
kuwepo na Utawala bora na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa
Wilaya ya Nyasa.
Kero zilizotolewa na watumishi wa Wilaya ya Nyasa
ni upandaji Madaraja, ulipwaji wa fedha za kujikimu wakati wa Uhamisho na
Likizo.
Aidha Katibu Mkuu amezichukua kero hizo kwa ajili
ya kuzifanyia kazi na kuzitatua Changamoto hizo kwa kuwa Serikali inawajali
watumishi wa Umma na wananchi kwa Ujumla.
Comments
Post a Comment