Na. Sekela Mwasubila, KONDOA
Waziri wa OR-TAMISEMI Mhe. Seleman
Jafo amewapongeza viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kondoa kwa
kusimamia vizuri miradi ya ujenzi wa madarasa na kuwataka kuongeza juhudi
katika kufanya kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma.
![]() |
Waziri Selemani Jafo |
Ameyasema hayo
wakati wa ziara yake ndani ya Halmashauri ya Mji Kondoa ya ukaguzi wa miradi na
kuongea na watumishi akiongozana na wataalam kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma.
“Kabla ya kuja
hapa nilipita katika miradi nimekagua jengo jipya la Halmashauri jengo ni zuri
hongereni linaendana na nyie ila lipo nyuma ya muda sijaridhika ikifika
Februari 1 nataka Mkurugenzi na watumishi wako mhamie kule lakini miradi ya
ujenzi wa madarasa ipo vizuri ila wakati mwingine mzingatie ushauri nilioutoa
ili tuwe na majengo yatakayodumu kwa mufa mrefu,” amesema Mhe. Jafo
Aidha
amewashauri kuongeza mapato kwa kubuni vyanzo vipya ambavyo havitawaumiza
wananchi ili kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kuiendesha Halmashauri na
kuondokana na utegemezi wa serikali japokuwa wanafanya vizuri katika ukusanyaji
wa mapato.
“Watumishi wote
fanyeni kazi kwa kujituma zaidi na mnapopewa kazi zifanyeni kwa wakati ila
kubwa fanyeni kazi kwa kupendana kwani muda mwingi watumishi mnautumia mkiwa
kazini katika baadhi ya maeneo watumishi wa idara moja hawaongei hii inapunguza
pia utendajikazi kwani wanaopendana hufanyakazi vizuri,” amesisitiza Mhe. Jafo
Aidha amewataka
Idara ya maendeleo ya Jamii kusimamia asilimia kumi za mapato na kuhakikisha
zinawafikia walengwa kwani katika baadhi ya maeneo fedha hizo zimekuwa
hazitolewi kutokana na wakurugenzi kuzuia fedha hizo kutoka na kuahidi
kusimamia mapitio ya kanuni za mikopo hiyo ili sehemu ya marejesho zitumike
kwaajili ya ufuatiliaji wa mikopo hiyo.
Hata hivyo
amewaagiza Makatibu Tawala wa mikoa kufanya tathmini ya bei za dawa kwa
mshitiri na bei ya soko ili dawa zipatikane vituoni na amemuagiza Mganga Mkuu
kufunga mfumo wa kielektroniki katika vituo vya afya na zahanati ili kuzuia
wizi wa dawa.
Akiongea awali
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Suleman Serea amemshukuru Mhe. Waziri kwa ziara yake
ndani ya mkoa wa Dodoma kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ambapo serikali imetoa
fedha nyingi za utekelezaji wa miradi na kumuahidi kusimamia maagizo yote
yaliyotolewa ili kuhakikisha huduma inatolewa kwa wananchi.
Akimkaribisha
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kondoa Mkurugenzi Msoleni Dakawa amesema
katika mwaka wa fedha 2017/18 halmashauri ilikisia kukusanya shilingi milioni
mia 800 lakini mpaka kufika mwisho wa mwaka wa fedha ilikusanya shilingi
bilioni 1.2 sawa na 133% na mwaka 2018/19 ilikisia kukusanya shilingi bilioni
1.6 mara mbili zaidi ya mwaka ulioisha na hadi kufikia 30 Juni 2019 Halmashauri
ilikusanya shilingi 1.4 sawa na 88% hata hivyo kutokana na changamoto
mbalimbali katika mwaka wa fedha 2020/21 imekisia kukusanya shilingi bilioni
1.4 na inaendelea kubuni vyanzo vingine vya mapato ili kukusanya mapato mengi
zaidi bila kumuathiri mwananchi.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kondoa, Mhe. Mohamed Kiberenge amemshukuru
Mhe. Waziri kwa kuwatembelea na kumuahidi kufanya kazi kwa kushirikiana na
Mkurugenzi na watumishi wote ambao ana imani kubwa nao kutokana na utendaji wao
mzuri kwa lengo la kuibadilisha Halmashauri ya Mji Kondoa.
Ziara ya Mhe.
Jafo imefanyika ikiwa ni mwendelezo wake wa kutembelea Halmshauri na kukagua
miradi ambapo alipata fursa ya kutembelea ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Mji
Kondoa lililoghalimu zaidi ya shilingi bilioni 3, ujenzi wa madarasa shule ya
Msingi Maji ya Shamba na Shule ya Sekondari Ula ikiwa ni kati ya shule 7
zilizopokea shilingi milioni 291 na kuongea na watumishi.
MWISHO
Comments
Post a Comment