TIJA KWENYE KILIMO NDIO KIPAUMBELE- PROF. MKENDA

Na. Mwandishi Wetu, DODOMA

Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda amesema kipaumbele chake ni kuona wakulima wanaongeza tija kwenye uzalishaji wa mazo nchini kwa kutumia eneo dogo kuzalisha mazo mengi zaidi na kukuza uchumi wa kaya na taifa.

 

Waziri wa Kilimo, Mhe. Prof. Adolf Mkenda ( kushoto) akipokea nyaraka za ofisi wakati alipokabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Vwawa Mhe.Japhet Hasunga halfailiyofanyika leo Mtumba Jijini Dodoma

Waziri wa Kilimo amesema hayo wakati akikakabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga hafla iliyofanyika makao makuu ya wizara ya Kilimo Mtumba jijini Dodoma.

Hafla ya makabidhiano imefanyika kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kumteua Prof. Mkenda kuwa Waziri wa Kilimo katika awamu hii ya pili ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano.

“ Sekta ya kilimo inachangia asilimia 28 ya pato la taifa lakini sekta ndogo ya mazao inachangia asilimia 18 ambapo tija ni ndogo. Tija kwenye kilimo ni ndogo sana wakati theluthi mbili ya watanzania inategemea kilimo kwenye maisha ambapo asilimia karibu 70 imejiali huko” alisema Prof. Mkenda.

Katika salamu zake Mhe. Hasunga amesema anamshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini na kumteua kuongoza wizara ya kilimo kwa miaka miwili ya awamu yake ya kwanza na kuwa alifanya  kazi kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula.

“Nimefanya kazi miaka miwili kama Waziri wa Kilimo, nafurahi  katika kipindi chote cha kwanza cha awamu ya tano nchi imeweza  kujitoshelevu kwa chakula” alisema Hasunga.

Hasunga alisema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiwango kikubwa na msukumo wa uongozi wa Rais Magufuli pamoja na wakulima wa Tanzania waliotikia kauli mbiu ya kufanya kazi kwa bidii.

Waziri huyo mstaafu na mbunge wa Jimbo la Vwawa mkoa wa Songwe aliongeza kusema ataendelea kuwa mwaminifu na kuiomba wizara ya kilimo kutilia mkazo suala la upatikanaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu bora, viuatilifu, mbolea na zana bora ili kilimo kikue na kuchangia zaidi kwenye pato la taifa.

 

Picha ya pamoja mara baada ya makabidhiano ya ofisi . Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ( wa pili toka kushoto) na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga ( katikati) ,Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kushoto wa kwanza) Wengine na Naibu Waziri Hussein Bashe ( wa pili toka kulia) na Naibu Katibu Mkuu Prof. Siza Tumbo ( kulia).

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda alisema atahakikisha sekta ya kilimo inaongeza kuchangia ukuaji wa uchumi toka wa sasa wa asilimia 28 hadi zaidi huku sekta ya kilimo mazao ikitoa mchango mkubwa kwenye upatikanaji wa maligahfi za viwanda.

 

Katika kuhakikisha sekta ya kilimo inatoa mchango mkubwa kwenye kwenye ukuaji wa uchumi nchi, Prof .Mkenda maetaja mambo makuu manne ambayo ni diara kwake wakati akiongoza Wizara ya Kilimo.

Kwanza kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa kutumia eneo dogo kuvuna mazao mengi hivyo taasisi ya utafiti (TARI) na wakala wa mbegu (ASA) wana jukumu la kuongoza kwenye utafiti wa mbegu bora nyingi ili wakulima wazalisha zaidi.

Pili, kusimamia na kuelimisha mbinu bora za uzalishaji (Good agricultural practices) ambapo amelenga kufanya umwagiliaji kwa njia ya matone ukue na kuchangia kwenye uhakika wa chakula ikiwemo upatikanaji wa viutalifu na huduma za ugani kwa karibu zaidi.

Mkakati wa tatu Prof. Mkenda ameutaja kuwa ni upatikanji wa masoko ya uhakika wa mazao ya wakulima kwa kusimamia masoko ya kimkakati na kufanya wakulima wanufaike na jasho lao kwa faida huku nchi ikiwa na uhakika wa chakula na malighafi.

Mwisho Prof Mkenda amesema katika uongozi wake ndani ya wizara ya Kilimo atahakikisha upatikanaji wa mitaji na uwekezaji kwenye kilimo unaluwa rahisi na wenye kunufaisha makundi ya vijana na wawekezaji ambapo atatoa mkazo kwenye upatikanaji wa mitaji kupitia miko yenye riba nafuu toka taasisi za fedha nchini na zile za nje ya nchi.

Ka upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alisema kuwa wizara hiyo inazo changamoto ikiwemo kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa upatikanji wa sukari ambapo wa sasa upungufu ni zaidi ya tani 60,000 kila mwaka na upande wa upatikanaji mafuta ya kula upungufu ni zaidi la tani 365,000.

Kusaya alitoa wito kwa viongozi wakuu wa wizara wapya kushirikiana na watumishi ili kuhakikisha lengo la serikali ya awamu ya tano la kufikia hekta milioni moja na laki mbili zinafikiwa na kufanya sekta hiyo ichangie zaidi kwenye ukuaji wa uchumi kwani Tanzania ina eneo la hekta milioni 29 zinazofaa kilimo cha umwagiliaji kati ya hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo.

Mwisho.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.