Na. Catherine
Sungura,WAMJW-Dodoma
Wataalam wa Maabara
nchini wametakiwa kuongeza kasi katika kuhakikisha huduma za tiba inayotolewa
inafuata miongozi ya wizara na kuhakikisha wanabadili fikra na mitazamo ili
kuwafanya wateja wao waweze kuvutiwa na huduma wanazozisimamia.
Hayo yamesemwa leo na
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba
Asili/Mbadala Dkt. Paul Mhame wakati wa kikao kazi cha
usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba katika ukumbi wa Chimwaga
jijini Dodoma.
Dkt. Mhame amesema kuwa
miongozo hiyo itakayowasilishwa kwa siku mbili imesisitiza kuboresha utoaji wa
huduma za tiba pia masuala ya usimamizi wa huduma za damu salama pamoja na
sheria, kanuni na miongozo ya kusimamia Tiba Asili nchini.
“Hakikisheni masuala
haya ambayo ni mtambuka katika utoaji wa huduma mnayaelewa vyema ili muweze
kuisaidia jamii, ikumbuke kuwa yapo maelekezo yaliyotolewa na viongozi wa
kitaifa hususan suala la tiba asili na tiba mbadala hivyo muhakikishe
mnawawezesha waratibu hao pindi inapotokea changamoto katika kusimamia huduma
hizi kwenye ngazi mnazosimamia”.Alisisitiza Dkt. Mhame.
Hata hivyo Dkt. Mhame
aliwataka washiriki hao kuhakikisha ujumbe utakaotolewa kwenye kikao kazi hiko
kitawafikia walengwa ili pindi ukaguzi na usimamizi shirikishi utakapofanyika
uwe na tija katika kuboresha huduma za tiba kwenye maeneo waliyotoka na hivyo
itasaidia kuboresha huduma za uchunguzi katika hospitali na ngazi mbalimbali za
utoaji huduma za tiba nchini.
Naye Mkuu wa huduma za
Maabara nchini kutoka Wizara ya Afya Peter Torokaa amewasisitiza vituo vyote
vya kutolea huduma za afya nchini kufanyia tathimini ya ufanisi “Calibration”
wa mashine zote kwa kuwatumia wataalam wa maabara na zile zinazotakiwa
kufanywa na Shirika la Viwango (TBS) wanafanyia pia kwani ndio wenye mamlaka.
Aidha, Torokaa amewataka
Mameneja na Waratibu wa maabara wa Mikoa na Wilaya kuhakiki uwezo wa mashine
“Method Verification” kupima na kutoa majibu yaliyo sahihi hivyo kila kipimo
kithibitishwe kama kinatoa majibu ya wagonjwa yaliyo sahihi.
“Jambo la tatu
tunalosisitiza ni wataalam wetu kupimwa umahiri kwa kuhakikisha mameneja na
waratibu wetu wa Mikoa na wilaya wanasimamia watoa huduma wetu ambao ni
wataalamu wa maabara wanafanyiwa umahiri kama wana uwezo wa kutumia hiyo
mashine,kifaa na kutoa majibu ikiwemo uwezo wa tafsiri majibu ambayo
yanaenda kwa Daktari kufanya maamuzi kwa mteja.
Aliongeza kuwa kila
kipimo lazima kifanyike kidhibiti ubora kabla maabara haijatoa majibu kwenda
kwa daktari kuhakikisha inadhibiti majibu hayo ndani ya maabara kwa kila kipimo
pamoja na kuhakikisha maabara inashiriki sampuli zingine ndani na nje ya
nchi ili kuweza kujipima kama wanaweza kutoa majibu yaliyo sawa.
Naye Meneja wa Maabara
wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga-Bombo Sinde Mtobu amesema maabara
yao imekuwa miongozi wa uboreshaji wa huduma nchini na kuwa katika ngazi
ya nyota nne hivyo wanasubiri kupata ithibati ya kimataifa IS0-15-18-9
kwenye huduma za ubora kwa ujumla hivyo wapo miongoni mwa maabara 27 nchini.
Ametaja moja ya
eneo ambalo wamefanya vizuri kwenye maabara ni kuwawezesha wataalam wa
maabara kwenye umahiri kwa kusimamia miongozo yote pamoja na eneo la uhakiki
ubora wa huduma zao kabla ya kwenda kwa daktari.
MWISHO
Comments
Post a Comment