NFRA Wajipange kununua Mahindi mengi kwa Wakulima – RC Wangabo

Na. Abdul Rahman Salim,

 

Wakati Utekelezaji wa lengo la Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) la kuweka mfumo wa kisasa wa kutunza mazao kufikia asilimia 80. Wakala hao wameshauriwa kujiandaa kununua mahindi mengi Zaidi ili kuwahakikishia wakulima soko la mazao yao katika kipindi cha msimu wa 2020/2021.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (aliyechuchumaa) akiangalia moja ya mfumo wa Kihenge kilichomalizika kujengwa katika ziara yake ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa vihenge hivyo akiwa na timu ya wataalamu wa Mkoa na Wilaya pamoja na NFRA


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema kuwa ni vyema NFRA wakaongeza fedha za kununua mahindi na kisha kutafuta soko nje ya nchi hasa katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Pamoja na nchi nyingine ili kuwapa fursa wakulima nchini kufanya biashara na NFRA ili kuepuka kuhangaika kutafuta soko la mazao yao.

“Mkoa wa Rukwa tumezalisha tani za mahindi tani 585,000 na matumizi yetu ya ndani ni tani 291,000 kwahiyo tulikuwa tuna ziada ya tani 294,000, sasa ukiangalia kwamba tani 294,000 halafu mahindi yananunuliwa tani 11,000 kwahiyo mahindi mengi yalibaki ndio kikawa kilio cha wakulima wa mkoa wetu wa Rukwa kwahiyo nategemea kwamba ukamilishwaji wa vihenge hivi NFRA itakuwa na uwezo wa kuchukua tani 58,500, hii kwa sisi mkoa wa Rukwa ni sawa na kuingiza na kutoa ili wawauzie watu wengine.”

“Kwahiyo niwaombe NFRA ndio wamekuwa mkombozi sasa kwa wakulima, mjipange vizuri ili kuongeza fedha muweze kununua mahindi mengi kwa wakulima vinginevyo wakulima watakata tamaa na sasa wanaendelea kuzalisha baada ya kuona kwamba hivi vihenge hapa vinakwenda kukamilika kwahiyo uwezo wa NFRA utakuwa mkubwa Zaidi wa kununua mahindi kwa wakulima, ninyi mnao uwezo wa kuona wapi muyapeleke hayo mahindi, ninyi mfanye biashara na nje na sisi tufanye biashara na nyie,” Alisema.



Kwa upande wake Mhandisi Mkazi kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mhandisi Haruna Kalunga amesema kuwa hadi tarehe 28.12.2020mkandarasi ameshatumia muda wake wa miezi 15 sawa na asilimia 83 ya muda aliopewa kwenye mkataba huku utekelezaji ukiwa ni asilimia 80 na hivyo kuufanya mradi kuwa nyuma kwa asilimia 3 na kuongeza kuwa ucheleweshwaji huo umechangiwa na kucheleweshwa kwa msamaha wa kodi wa vifaa vinavyotoka nje ya Tanzania.

Kwa mkoa wa Rukwa mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Unia Araj kutoka Poland ikisaidiana na Mkandarasi Mzawa Elerai kutokea Arusha kwa thamani ya Dola za marekani 6,019,399.00 ambayo ni asilimia 30 ya mradi mzima unaotekelezwa katika mikoa mitatu Pamoja na Mkoa wa Katavi na Manyara wenye jumla ya thamani yad ola za marekani 20,280,906.00.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.