Na. Mwandishi Wetu,
TIMU ya Dodoma Jiji FC iliyo chini ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kesho
Ijumaa Januari 1, 2021 siku ya mwaka mpya itakuwa kibaruani ugenini kwa mara
nyingine kuikabili Mwadui FC ya Shinyanga kwenye dimba la Mwadui Complex majira
ya saa 8:00 mchana katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa ligi kuu ya
soka ya Tanzania Bara.
Mchezo uliopita Dodoma Jiji iliitandika Mtibwa Sugar ya Morogoro bao 1-0
kwenye uwanja wa Jamhuri Manispaa ya Morogoro na sasa imehamishia makali hayo
huko kwenye machimbo ya almasi ya Mwadui huku ari kikosini ikiwa juu kusaka
pointi tatu za msingi.
Tayari kikosi cha wachezaji 20 na viongozi 8 kipo mkoani Shinyanga na leo
Alhamisi Disemba 31 mchana kinatarajiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja
huo ili kuzoea hali ya hewa kwa sababu mchezo huo utaanza saa 8:00 mchana kwa
majira ya Tanzania.
Dodoma Jiji FC imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya 8 kwenye
msimamo wa ligi hiyo yenye timu 18 na inahitaji ushindi kwa udi na uvumba ili
kuendelea kujiweka sehemu salama kwenye msimamo wa ligi hiyo wakati huu ambapo
mshambuliaji wake Seif Abdallah Rashid Karihe akiwa amewasha moto kwenye
kufumania nyavu akiwa amefunga katika michezo minne mfululuzo akiwa na magoli
matano licha ya kusumbuliwa na majeraha na kukosa mechi za mwanzo wa msimu.
Wakati Karihe akitikisa nchi katika ufungaji, safu ya ushambuliaji
itaongezewa makali na urejeo wa mshambulizi Anuar Jabiri ambaye alikuwa na
majukumu ya nchi katika timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 maarufu
Ngorongoro Heroes sambamba na beki wa kulia Anderson Solomoni.
MWISHO
Comments
Post a Comment