TAMKO KUHUSU SIKU YA MATUMIZI YA CHOO DUNIANI NA WIKI YA USAFI WA MAZINGIRA TANZANIA TAREHE 16-19 NOVEMBA, 2020 LILILOTOLEWA NA PROF. MABULA D. MCHEMBE, KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO MNAMO TAREHE 19 NOVEMBA, 2020
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
Ndugu Wanahabari,
Nina
kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha sisi sote kuwepo
mahali hapa siku ya leo huku tukiwa na afya njema kwa ajili ya kuzungumzia
suala hili muhimu. Ninapenda pia kuwapongeza nyote kwa jinsi mlivyoshiriki
katika zoezi la uchaguzi wa kihistoria kwa nchi yetu ambapo serikali ya awamu
ya tano chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeingia madarakani kwa muhula wa pili. Hii ni hatua kubwa
na ya kujivunia kwa Taifa letu kwani tumeidhihirishia dunia kuwa Watanzania ni
wapenda amani na tunaheshimu Demokrasia. Leo tunakwenda kuzungumzia kuhusu Siku
ya Matumizi ya Choo Duniani na Wiki ya Usafi wa Mazingira Tanzania.
Ndugu Wanahabari,
Tarehe
19 Novemba kila mwaka ni kilele cha Wiki ya Usafi wa Mazingira Kitaifa ambayo
pia ni Siku ya Matumizi ya Choo Duniani yaani World Toilet Day. Lengo la Maadhimisho ya Wiki ya Usafi wa
Mazingira Kitaifa ni kuikumbusha jamii kuendelea kuzingatia Sheria na Kanuni za
Afya ikiwa ni hatua muhimu ya kujikinga na maradhi yanayoenezwa kwa njia ya
uchafu. Aidha, kuweka msukumo kwa wadau na kuongeza kasi ya utekelezaji wa
huduma za afya mazingira katika kuboresha afya ya jamii. Wiki ya Usafi wa
Mazingira ni mojawapo ya mikakati mahususi ambayo inatumika kuibua na kuongez a
uelewa kuhusu umuhimu wa usafi katika ustawi wa jamii hasa katika nyanja za
Afya, Maji, Elimu na Uchumi. Umuhimu wa maadhimisho haya unatokana na ukweli
kwamba suala la upatikanaji wa huduma bora za usafi wa mazingira bado ni
changamoto kubwa Kitaifa na Kimataifa. Kwa mfano, takribani watu bilioni moja
duniani kote hawana huduma ya choo kabisa na kwamba watu wengine bilioni 2.5
sawa na theluthi ya watu wote duniani hutumia vyoo duni (asili).
Ndugu Wanahabari
Wiki
ya Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2020 itaadhimishwa Kitaifa kuanzia tarehe 16-19
Novemba, ambapo wataalam na wadau wa masuala ya Usafi wa Mazingira nchini
watajumuika katika kutoa elimu kwa jamii, kufanya shughuli za usafi katika
maeneo mbalimbali ya umma, kufanya ukaguzi wa maeneo ya makazi na biashara
pamoja na kushiriki katika mikutano ya kisayansi yenye lengo la kuongeza uelewa
juu ya masuala ya wa Afya Mazingira nchini.
Kaulimbiu
ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Zingatia
Mahitaji ya Jinsia kwa Usafi wa Mazingira Endelevu” (Gender Consideration a Pillar for sustainable Sanitation and Hygiene)
Kaulimbiu
hii inalenga kuongeza uelewa zaidi juu ya umuhimu wa kujenga na kutumia choo
bora pamoja na kuweka mazingira katika hali ya usafi wakati wote mustakabali wa
matumizi sahihi kwa kuzingatia jinsi. Kila kaya nchini inatakiwa kujenga na
kutumia vyoo bora pamoja na kunawa mikono ili kujilinda na magonjwa. Ikumbukwe
kwamba, jamii inapotumia maeneo mengine kujisaidia badala ya kutumia vyoo tunasababisha
uchafuzi wa mazingira hususani vyanzo vya maji na kupelekea vimelea vya
magonjwa ambavyo ni hatari kwa afya zetu na kutuathiri sisi wenyewe. Hivyo,
jukumu la kuhakikisha jamii inajenga na kutumia vyoo bora ni la kila mmoja wetu
ili kujilinda na magonjwa yanayoenezwa na uchafu.
Ndugu Wanahabari,
Lengo
la 6.2 la maendeleo endelevu limeweka bayana kuwa ni kuhakikisha kila mtu
duniani ananga na kutumia choo bora na kufikia mwaka 2030 hakuna atakayejisaidia
hovyo katika mazingira yasiyo rasmi (nje ya choo). Kwa upande wa hapa nchini kaya
zenye vyoo bora zimeongezeka kutoka asilimia 59 mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 63.7 mwezi Juni, 2020. Mikoa
inayoongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya kaya zenye vyoo bora ni Dar es Salaam
(95.8%), Iringa (77.5%) na Njombe (74.6%). Mikoa yenye hali duni ni Kigoma (49.3%),
Lindi (49.2%) na Dodoma (46.1%).
Ndugu Wanahabari,
Ni
jukumu la kila sekta kuhakikisha kuwa ufuatiliaji wa kina unafanyika katika
ngazi zote kuanzia kaya, shule, vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na taasisi pamoja na vituo vya mabasi ili kutilia
mkazo kuhusu ujenzi na matumizi ya vyoo bora. Ni muhimu kila kaya kuhakikisha
inajenga na kutumia choo bora ili kuondokana na magonjwa yanayotokana na uchafu
yakiwemo magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Ndugu Wanahabari,
Ninapenda kuchukua fursa hii kuhimiza mambo yafuatayo:-
1. Jamii ihakikishe inajenga na kutumia vyoo bora.
2. Kujenga tabia ya kunawa mikono pamoja na kuimarisha usafi wa mazingira
ngazi ya kaya;
3. Wazazi na walezi wahakikishe wanatupa kinyesi cha
watoto chooni pamoja na kunawa Mikono kwa maji na sabuni ;
4. Taasisi, maeneo ya umma, maeneo ya biashara za vyakula
zihakikishe uwepo wa vyoo bora pamoja na sehemu maalum za kunawa mikono kwa
maji tiririka na sabuni kwa rika zote.
5. Kila kaya na maeneo yote yahakikishe yanakuwa na vyoo
bora na vifaa vya kunawia mikono
Ndugu Wanahabari,
Kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya usafi na siku ya
matumizi ya choo duniani, Wizara inaelekeza Sekretarieti za Mikoa pamoja na Mamlaka
za Serikali za Mitaa kutekeleza yafuatayo:-
1. Kuratibu
shughuli za utoaji wa elimu ya afya kwa jamii kwa kutumia vyombo vya habari
vilivyoko katika Mikoa na Halmashauri ili kuisisitiza jamii kuhusu ujenzi na matumizi ya vyoo
bora pamoja na umuhimu wa kunawa mikono
kwa maji tiririka na sabuni;
2. Kushirikisha
viongozi mbalimbali kwenye Mikoa wakiwemo viongozi wa Dini, Wanasiasa na watu
maarufu katika kutoa elimu ya ujenzi na matumizi ya vyoo bora kwa jamii;
3. Wadau
wote wa masuala ya Afya Mazingira na usafi kote nchini washirikiane na Serikali
katika kutoa elimu na kuhamasisha mabadiliko ya tabia kuhusu matumizi ya vyoo
bora pamoja na unawaji wa mikono;
4. Kufanya
kaguzi kwenye vituo vya abiria (hasa mabasi yaendayo Mikoani), taasisi za umma
na binafsi, maeneo ya biashara pamoja na jumuiya ili kuhakikisha uwepo wa vyoo
bora pamoja na vifaa vya kunawa mikono na sabuni.
5. Matumizi
ya sheria kwa wakiukaji wote wa kanuni za afya
Ndugu Wanahabari,
Siku
zote tunasisitiza kwamba Kinga Ni Bora Kuliko
Tiba hivyo wito wangu kwa jamii ni kuhakikisha tunajenga na kutumia vyoo
bora pomoja na kunawa mikono kwa maji tirirka na sabuni ili kulinda afya zetu. Ni
mategemeo yangu kuwa jamii kwa ujumla wake italipa kipaumbele suala la usafi wa
mazingira pamoja na matumizi ya vyoo bora na kulifanya kuwa mojawapo ya tabia
ya kudumu kwa kila mtu.
Ninawashukuru
kwa kunisikiliza.
Comments
Post a Comment