Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa
Siku 60 kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA)
kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa kijiji cha Litisha katika Halmashauri ya
wilaya ya Songea.
Mhandisi Sanga ameelekeza hayo Novemba 28, 2020 wakati wa
ziara yake ya kukagua na kujionea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa miradi ya maji
inayotekelezwa wilayani humo akiwa ameambatana na Mbunge wa Jimbo la Peramiho,
Jenista Mhagama.
Akiwa kwenye mradi wa maji wa Litisha unaotekelezwa na wataalam wa ndani kutoka SOUWASA, Mhandisi Sanga alijionea hali halisi ya ujenzi wake ambapo alisema amefarijika kuona kisima kilichochimbwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa kijiji hicho kikitoa maji mengi.
Hata hivyo alisisitiza ukamilishwe haraka na huku akikumbushia dhamira ya Serikali ya kuwasogezea huduma ya maji wananchi wakehasa wanyonge ili kuwapunguzia usumbufu wa kutembea umbali mrefu kufuatilia huduma ya magi.
“Nimefurahi kuonakisima kinatoa maji mengi sana na tenki tayari limekamilika lakini bado miundombinu ya kuwafikishia wananchi maji haijakamilika; maelekezo yangu ni kuwa, ndani ya siku 60 mradi huu uwe umekamilika na wananchi wawe wamepata huduma ya maji,” alielekeza Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga aliwahakikishia wananchi wa Songea kwamba
Serikali haitowaangusha, itahakikisha huduma ya majisafi na salama inawafikia
wananchi mapema iwezekanavyo kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha
Mapinduzi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
“Ninawahakikishia Serikali mliyoichagua kwa kura nyingi
haitowaangusha, iliahidi na sasa inatekeleza, ni suala la muda tu, kero ya maji
hapa Litisha na maeneo mengine ya jimbo hili la Peramiho tunakwenda kuimaliza,”
alisisitiza Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga alibainisha kwamba kabla ya mwezi huu
kumalizika Wizara ya Maji itapeleka kiasi cha shilingi milioni 200 ili
kuiwezesha SOUWASA kununua mabomba sambamba na kuhakikisha huduma ya nishati ya
umeme imefika kwenye mradi ili wananchi wapate huduma.
“Tutaleta milioni 200 kwa ajili ya kununua mabomba na kujenga
miundombinu ya kuwasogezea huduma wananchi wanyonge ili ndani ya siku 60, wawe
wamefikishiwa maji,” alisisitiza Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista
Mhagama kwa jitihada zake za kufuatilia utekelezwaji wa miradi ya maji jimboni
humo.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi kwenye halmashauri ya
wilaya ya Songea, Mkurugenzi Mtendaji wa SOUWASA, Mhandisi Patrick Kibasa
alisema inatekelezwa kupitia Fedha za Mfuko wa Maji na inahusisha uchimbaji wa
visima virefu na ujenzi wa miundombinu ya maji.
Kibasa alisema miradi inatekelezwa kwa awamu mbili tofauti na
kwamba awamu ya kwanza inatekelezwa kupitia Mkandarasi Drilling and Dam
Construction Agency (DDCA) na inahusisha uchimbaji wa visima virefu 39 katika
vijiji 20 vya Halmashauri ya Wilaya ya Songea na kwamba tayari visima 19
vimechimbwa na shughuli inaendelea.
Aidha, aliongeza kuwa awamu ya pili inatekelezwa na wataalam
wa ndani na inahusisha ujenzi wa miundombinu ya maji kwenye vijiji nane
vilivyothibitika kuwa na maji ya kutosha na kwamba ujenzi umeanza katika vijiji
vinne ambavyo ni Litisha, Litowa, Nakahuga na Peramiho B kwa gharama ya
shilingi bilioni 2.4
MWISHO.
Comments
Post a Comment