![]() |
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama
(IJA) Lushoto, Mhe. Jaji.Dkt. Paul Kihwelo akifungua Mafunzo ya Madalali
na Wasambaza Nyaraka za Mahakama yanayofanyika katika
ukumbi wa Chipeta uliopo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo
Dar es Salaam. Kushoto ni Mratibu wa mafunzo hayo, Bi. Hamisa Mwenegoha.
Na: Rosena Suka
IJA
Madalali na Wasambaza Nyaraka wa
Mahakama ya Tanzania kutoka maeneo mbalimbali ya nchini wanashiriki katika
mafunzo ya wiki mbili yanayoendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ili kuhakikisha kuwa Mahakama inakuwa na Madalali na Wasambaza Nyaraka
wenye mbinu bora na nyenzo za kufanyia kazi.
Akifungua Mafunzo hayo yanayoendelea katika ukumbi
wa Chipeta uliopo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo, Mkuu
wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo amewataka
Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuwa na mijadala huru itakayosaidia
kuboresha utendaji kazi wao ili kupunguza malalamiko yanayotokana na wananchi
kutokupata huduma bora.
Mafunzo haya yamekusanya zaidi ya washiriki 40 kutoka
katika sekta mbalimbali za umma na
binafsi. Akielezea lengo kuu la mafunzo hayo, Mhe. Dkt. Kihwelo amesema endapo
Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama watalalamikiwa kwa kutokuwatendea
haki wananchi ni dhahiri kuwa Mahakama pia itakuwa imelalamikiwa kwa kuwa watu
hao hufanya kazi na Mahakama.
“Kuanzishwa kwa mafunzo ya Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama ni mojawapo ya sehemu ya maboresho makubwa yanayoendelea katika muhimili wa Mahakama,” alieleza Mkuu huyo wa Chuo.
Mhe. Kihwelo aliongeza kuwa mafunzo haya yanafanyika ili kuondoa malalamiko mengi yaliyokuwepo kutoka kwa wananchi ambapo kwa kufanya hivi itawawezesha Madalali na Wasambaza Nyaraka kufanya kazi kwa kufuata kanuni zilizopo.
![]() |
Sehemu ya washiriki wakifuatilia
Mafunzo
Naye, Mratibu wa mafunzo hayo, Bi. Hamisa Mwenegoha alisema mafunzo hayo ambayo yalianza Novemba 23, 2020 na kutarajiwa kuhitimishwa Desemba 04 mwaka huu yanafanyika kwa mara ya sita ili kuendelea kuwajengea uwezo na kukuza taswira nzuri ya Mahakama ya Tanzania.
Kwa upande mwingine, Bi. Mwenegoha alisema sheria inaweka masharti kwa Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuhuisha leseni za kufanyia shughuli hizo ili kutimiza matakwa ya sheria inayoongoza shughuli zao. Pamoja na mambo mengine, sheria imeweka vigezo vya mtu mwenye kufanya shughuli hizo ambapo moja ya vigezo hivyo ni kupatiwa mafunzo ya umahiri kutoka chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Mafunzo mengine ya aina hiyo yatatolewa katika vipindi tofauti tofauti kwa lengo la kumpa fursa mtu yeyote mwenye vigezo stahiki kupatiwa mafunzo maalum yatakayomwezesha kupata cheti cha umahiri katika udalali na usambazaji nyaraka za Mahakama Pamoja na kuifanya kazi hiyo kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kisheria zilizopo.


Comments
Post a Comment