Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Mh. Joachim Wangabo amewaagiza wakuu wa Wilaya Mkoani humo kusimamia tathmini
ya utekelezaji wa mkakati wa miaka mitano (2020 -2025) wa kukabiliana na mimba
za utotoni ifikapo mwezi Januari mwaka 2021.
Mh. Wangabo ameagiza
kuwa tathmini hiyo ifanyike mwezi Januari 2021 katika ngazi ya Wilaya na Mwezi
Februari, 2021 katika ngazi ya Mkoa ili kubaini mafanikio yaliyopatikana katika
kipindi cha mwaka mmoja tangu mkakati huo kuzinduliwa tarehe 18.2.2020.
Aidha, alitaja baadhi
ya mambo muhimu aliyowasainisha wakuu hao wa wilaya kuwa ni Pamoja na ujenzi wa
shule za msingi kwa kila Kijiji, chakula mashuleni, ujenzi wa mabweni ya
wasichana katika shule za sekondari na kila kata kuwa na shule yake ya
sekondari.
Mh. Wangabo ametoa
maagizo hayo leo tarehe 26.11.2020 wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kuzuia Ndoa
na Mimba za Utotoni Mkoani Rukwa unaotekelezwa na Shirika la Plan International
wakishirikiana na mashirika ya PDF, YES TZ, RUSUDEO na RAFIKI SDO huku ukiwa na
lengo la kuwawezesha Watoto wa kike kutambua haki zao, kujikinga dhidi ya ndoa
za utotoni, kuimarisha mifumo ya ulinzi na haki kwa Watoto Pamoja na
kukabiliana na mila potofu.
“Ni matarajio yangu kwamba mradi huu wa kuzuia ndoa na mimba
za utotoni mkoani Rukwa, utaleta mabadiliko makubwa kupitia afua na jumbe
mbalimbali zilizoandaliwa kupitia elimu ya Afya ya Uzazi na makuzi kwa vijana
ya nje na ndani ya shule, ufuatiliaji wa uanzishwaji wa mabaraza ya Watoto,
Uwezeshwaji wa miradi midogo midogo kwa wasichana na jamii kiuchumi, mabadiliko
ya mila na desturi potofu na uimarishaji wa mifumo ya ulinzi na utetezi wa
Watoto katika jamii kwa kipindi chote cha miaka mitano cha utekelezaji wa
mradi.”
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Plan International Laurent Wambura alisema kuwa ndoa za utotoni zimeendelea kusababisha
madhara kwa Watoto hasa wasichana kwa kukosa nafasi ya kuendelea na elimu,
kupata mimba katika umri mdogo, maambukiii ya magonjwa ngono, unyanyasaji wa
kijinsia na kingono, vifo visivyotarajiwa wakati wa kujifungua, pia uchumi
dhaifu, utegemezi na umasikini
“Ndoa pamoja na mimba za utotoni zimeendelea kuwa ni moja ya
changamoto katika kufikia ustawi wa mtoto wa kike hava Tanzania. Katika
Tanzania Demographic and HealthSurvey (TDHS) va mwaka 2016, asilimia 36% ya
wanawake kati ya miaka 20 hadi 24 waliolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka
18. Tafiti hii ya TDHS 2016 inaonyesha ongezeko la ndoa za utotoni hasa kwa
wasichana kati ya miaka 15 na 19 kwa asilimia 5% kutoka utafiti TDHS wa mwaka
2010,” Alisema.
Halikadhalika,
miongoni mwa watu waliohudhuria katika uzinduzi huo alikuwemo Farida Robert
ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mradi huo ulioanza utekelezaji wake mwezi
Januari 2020 na kutegewa kumalika mwezi Disemba 2024, naye alisema.
“Kwa mimi kama mimi
nimenufaika san ana huu mradi wa Plan International kwa kuletwa kwentu sisi
vijana, maana ni vitu vingi sana vinatokea kwetu vijana kama vile kukosa
mahitaji maalum kwa sisi vijana kama vile mavazi na chakula, huu mradi
umetunufaisha, umeweza kutuinua kutoka hatua moja hadi nyingine, mimi sasa
nashona, napata hela yang una inanisaidia kama msichana na siwezi kutekwa
kimapenzi na vijana wa kiume.”
Wakati akizungumza kwa
niaba ya Wakuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alisema kuwa
mradi huo katika awamu ya kwanza ulianza na kata tatu katika wilaya ya Nkasi na
mafanikio makubwa yalipatikana na hatimae awamu hii ya pili unatekelezwa katika
mkoa mzima na hivyo aliliomba shirika la Plan International kuona namna ya
kuchukua kata 27 za wilaya hiyo badala ya kata 15.
“Maombi yangu kwa Plan
international wakati hawa wengine wanapewa hizi kata sisi tungezimaliza kata
zote za wilaya ya Nkasi kama shukrani kwa namna ambavyo tulishiriki katika
mradi huu, kwa mfano kata kama Mkinga, Kipili ambazo hazimo katika orodha hii
ni maeneo ambayo nilitoa maoni sana kwamba mimba za utotoni na Watoto kuacha
shule ni maeneo ambayo yameathirika sana, tulitegemea awamu hii yangepewa
kipaumbele, nIna Imani changamoto hii wenzetu mtaishughulikia,” Alisisitiza.
Mh. Wangabo amezindua
mradi huo ikiwa ni mwendelezo wa kutekeleza mkakati wa miaka mitano (2020 –
2025) wa kukabiliana na mimba za utotoni Mkoani humo kama alivyoahidi katika
salamu zake za kufunga mwaka 2019 kuwa mwaka 2020 utakuwa ni mwaka wa mtoto
mkoani Rukwa huku mradi huo ukilenga kuwafikia Watoto 32,167; wasichana wakiwa
22,356 na wavulana 9,811. Pia walezi na wazazi 21,881 katika wilaya 3, Kata 36
na vijiji 116.
Comments
Post a Comment