KUTOKAMILIKA KWA UPELELEZI ISIWE SABABU YA KUCHELEWESHA MASHAURI: JAJI MKUU

Na Magreth Kinabo na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mahakimu nchini kutochelewesha mashauri bila sababu za msingi ikiwemo kutumia kigezo cha kuchelewa kukamilika kwa upelelezi kama sababu mojawapo bali watumie mamlaka yao ya Kikatiba kuhakikisha kuwa mashauri yanasikilizwa na kuamuliwa kwa wakati.

Baadhi ya Mahakimu Wakazi wapya wakila kiapo mbele ya Mhe. Jaji Mkuu


Mhe. Jaji Mkuu ameyasema hayo mapema leo Novemba 27, 2020 katika hafla fupi ya kuapishwa kwa Mahakimu  Wakazi  wapya 39 iliyofanyika kwenye ukumbi namba  moja wa Mahakama Kuu-Dar es Salaam, ambapo amesema  kumekuwa na malalamiko ya ucheleweshaji  bila sababu za msingi.

“Mahakama bado haizungumziwi na kutazamwa vizuri kuhusu ucheleweshaji wa maamuzi. Eneo hili   wananchi wanalalamika sana, na wanayo sababu za kulalamika hasa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi—ni ucheleweshwaji mkubwa wa kesi kubwa kubwa za mauaji, madawa ya kulevya, nyara za serikali, uhujumu uchumi, ugaidi, utakatishaji wa fedha,” alisema Mhe. Jaji Mkuu. 

Mhe. Jaji Prof. Juma aliongeza kwa kusema kuwa Mahakimu wanafanya kosa kubwa la kukubali Maahirisho yasio na kikomo na bila kupokea sababu zozote za msingi, huku akisisitiza kuwa sababu ya upelelezi unaendelea si ya msingi.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu alieleza kuwa wananchi wanalalamika ya kuwa, waendesha mashtaka wanatumia ucheleweshaji Mahakamani kama adhabu kabla hata kosa halijathibitishwa Mahakamani.

 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Mahakimu Wakazi wapya wa Mahakama za Mwanzo 39 (hawapo pichani) aliowaapisha mapema Novemba 27, 2020. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi na kulia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Lameck Mlacha

Aliongeza kwamba ili kuziba mwanya uliokuwa unatumiwa na Waendesha Mashtaka na Wapelelezi wa kuomba maahirisho yasio na kikomo, Mhe. Jaji Kiongozi alitoa  waraka namba  5 wa mwaka  2019, kuhusu  kuharakisha  Committal Proceedings, Plea Taking na Preliminary Hearing” na kuwataka Majaji na Mahakimu  kuusoma waraka huo kama mwongozo wa uendeshaji wa mashauri.

Mahakama nyingi zinakiuka sheria kwa kutotekeleza masharti ya Usimamizi wa Mirathi kwakushindwa kuhakikisha kuwa majalada ya mirathi yanafungwa kwa wasimamizi kuwasilisha mahesabu.

Aidha, aliwataka mahakimu hao kufuata utaratibu mwepesi wa kisheria ili Wasimamizi wa Mirathi wasitumie vibaya mali na kupora mali za marehemu.

Alisema   kwa mujibu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Ibara ya 107B, imewahakikishieni nyie Mahakimu (Pamoja pia na Wasajili, Majaji) kuwa, katika kutimiza ahadi ya viapo/vithibitisho vyenu-

“Mtatekeleza mamlaka ya utoaji haki, kupitia Mahakama zitakazokuwa huru na mtalazimika kuzingatia tu, masharti ya Katiba na yale ya Sheria za Nchi,” alisema. Huku akisisitiza kuwa maana yake ni kwamba, waongozwe na Katiba, Sheria na taratibu za kimahakama katika kazi za Uhakimu. Uhakimu wako utaimarika endapo siku zote utazingatia Sheria, na kuongozwa na taratibu, kanuni na nyaraka  zinazotolewa mara kwa mara na viongozi wa Mahakama. 

Pia aliwataka kunzingatia maadili ya kazi zao na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

 


Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.