Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kurejesha mali za vyama vikuu vya ushirika Nyanza, Geita na Simiyu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 61 zilizokuwa zikilikiwa kinyume cha utaratibu.
Akikabidhi hati 37 kwa wenyeviti wa vyama vya
Nyanza (NCU),Geita (GCU) na Simiyu (SIMCU) leo jijini Mwanza Katibu Mkuu Wizara
ya Kilimo Gerald Kusaya amesema kazi hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais
Dkt.John Pombe Magufuli aliyoyatoa mwezi Agosti mwaka 2016.
“Leo nimekabidhi hati miliki 37 zinazojumuisha
ardhi, majengo na mitambo yenye thamani ya shilingi Bilioni 61 zilizoporwa
kinyemela na watu kutoka vyama vya ushirika Nyanza, Geita na Simiyu ambao ndio
walikuwa wamiliki halali” alisema Kusaya.
Kusaya aliongeza kusema kazi hiyo ya kufuatilia na
kurejesha mali imefanywa na Timu Maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa mwaka 2016 baada ya agizo la Rais Magufuli alipofanya ziara mkoani
Mwanza kuwa mali zote za chama kikuu cha ushirika Nyanza zifuatiliwe na
kurejeshwa toka kwa waliozimiliki kinyume cha utaratibu.
Ili kuhakikisha wanaushirika wananufaika na mali
zao Katibu Mkuu Kusaya ametoa maagizo kwa viongozi wa vyama vya ushirika nchini
kuwa kurejeshwa kwa mali hizo zitumike kwa manufaa ya wakulima ambao ndio
wamiliki.
Pili, Mrajis wa Ushirika nchini ahakikishe mali
zilizorejeshwa zinakuwa salama na kuwa asitokee kiongozi yeyote atakayefanya
ubadhirifu.
Tatu, kwa watu wote ambao bado wanamiliki
zilizokuwa mali za ushirika kinyume cha utaratibu wazirejeshe mara moja kwa
serikali kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa kupitia Timu Maalum ya Waziri
Mkuu.
“ Nyanza kuna jengo lipo Nansio Ukerewe linaitwa
Pamba Hostel imebainika mkataba wake na Saad Songolo ulikiukwa. Tunataka
lirudishwe Serikalini, hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tunaomba uruhusu vyombo vya
dola vifanye kazi yake ili mali hii ya wakulima irejeshwe” alisema Kusaya.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John
Mongela ametoa pongezi kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa kwa uthubutu wao na uzalendo wa kutaka mali zote za wanashirika
zilizochukuliwa kinyemela kurejeshwa kwa wamiliki ambao ni wakulima.
Mongela alisisitiza kuwa mkoa wa Mwanza tangu agizo
lilipotolewa viwanja vya Furahisha tarehe 11 Agosti, 2016 umeshirikiana na Timu
Maalum ya Waziri Mkuu kwenye ufuatiliaji na hatimaye kufanikiwa leo kurejesha
mali hizi 27 za chama kikuu cha Nyanza na zingine za Simiyu na Geita.
“Leo tunamshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli
kwa kuwajali wakulima, wafugaji na wavuvi wa nchi hii hata kuagiza uchunguzi wa
mali zao zilizoporwa na wajanja wachache kwenye ushirika” alisisitiza Mongela
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Mwanza John
Mongela alimpongeza Mwenyekiti wa kwanza wa Timu Maalum ya Waziri Mkuu ambaye
sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya kwa kazi nzuri ya kufuatilia
urejeshwaji mali hizo kazi iliyokamilisha na timu ya pili chini ya Asangye
Bangu.
Aidha Mongela ametoa onyo kwa Viongozi wa Nyanza
Cooperative Union kuwa wasimamie vizuri mali hizi ili zisije tena kuuzwa kwa
watu kinyume cha utaratibu na kuwa sasa
Nyanza inatakiwa kuwa na Mtendaji Mkuu mwenye weledi na ujuzi wa kusimamia
ushirika.
Mongela ameiomba wizara ya kilimo “ ifanye kazi ya
kuhakikisha vyama vikuu vya ushirika vinapata na kuajili mameneja wakuu wenye
weledi, taaluma, ujuzi na uadilifu kuongoza ushirika ili vijiendeshe kibiashara
badala ya kutumia uzoefu tu usio na tija” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Akiwasilisha taarifa Mwenyekiti wa Timu Maalum ya
Waziri Mkuu Asangye Bangu alisema mali
hizo zilizorejeshwa ni sehemu ya zoezi endelevu la kufuatilia watu wote
waliojimilikisha au kuuziwa zilizokuwa mali za ushirika kinyume cha utaratibu.
Bangu alitaja mali zilizorejeshwa kwa vyama vikuu
vya ushirika Nyanza kuwa ni 27, Geita 9 na Simiyu 2 zikiwamo viwanja, majengo
na mitambo na kuwa timu yake inaendelea kufuatilia mali zingine kwenye vyama
hivi na vingine ikiwemo Kilimanjaro( KNCU) Shinyanga (Shirecu) na maeneo
mengine.
Akitoa shukrai kwa niaba ya wanaushirika nchini
Mrajis wa Ushirika Dkt. Benson Ndiege alisema kurudishwa kwa mali za ushirika kutasaidia kufufua na
kuimarisha utendaji kazi wa vyama vya ushirika nchini.
Dkt. Ndiege alisema atahakikisha mali zilizorejeshwa
zinatumika kwa manufaa ya wakulima ili ziwasaidie kuondokana na umasikini wa
kipato .
.
Mwisho
Imetolewa na;
Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
MWANZA
23.11.2020
Comments
Post a Comment