Viongozi wa dini Rukwa watahadharisha fujo siku ya Uchaguzi huku wakiliombea Taifa

Na. Abdul Rahman Salim, RUKWA

Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Rukwa kupitia Kamati ya Amani ya Mkoa huo wamewatahadharisha wananchi hasa kundi la vijana kuachana na fikra za kuanzisha ama kuchochea fujo katika siku ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika kesho tarehe 28.10.2020.

 

Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo akimsalimia Shekhe wa Wilaya ya Sumbawanga Rajab Stima muda mfupi baada ya kumaliza dua maaalum ya kuliombea taifa kuwa na uchaguzi mkuu wa amani na utulivu

Viongozi hao kwa nyakati tofauti wameyasema maneno hayo katika siku ya maalum iliyoandaliwa na Kamati hiyo ya Amani mkoani humo ili kuliombea taifa amani na kuuombea uchaguzi huo ufanyike kwa utulivu huku wakiwasihi wananchi kushiriki katika uchaguzi huo na kuondoka katika kituo cha uchaguzi mara tu baada ya kumaliza zoezi la kumchagua wanayemwona anafaa kuwaongoza kuanzia ngazi ya Kata, Jimbo na Nchi.

Wakati akitoa nasaha zake Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Rukwa, Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Ziwa Tanganyika Mkoani Rukwa aliwaomba wananchi kuwachagua viongozi watakao ipeleka nchi ya Tanzania inapotakiwa kwenda na sio viongozi wanaoleta mizaha katika maendeleo ya nchi.

“Kwahiyo siku hiyo tupige kura tuwachague viongozi ambao wanatokana na kiti cha enzi cha Mungu mwenyewe, Mungu ameshajichagulia viongozi katika taifa hili, sisi tutathibitisha kwa kura zetu na Mungu apate kutukuzwa na abaki katika nchi ya Tanzania ipate kusonga mbele,” Alisema.

Naye Kiongozi wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) Mkoani Rukwa, Sheikh Rashid Akilimali alisema kuwa vijana wa hivileo hawajawahi kushuhudia kutoweka kwa amani na kusahau kuwa kuna nchi za jirani ambazo waliwahi kushuhudia kutoweka kwa amani y ana matokeo yake walikimbilia nchini kwetu Tanzania kwaajili ya hifadhi na hivyo kuiomba serikali kuhakikisha vijana watakaosababisha fujo warudishwe katika mstari.

Kiongozi wa Baraza la Kuu Waislam Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Rukwa Shekhe Rashid Akilimali
 

“Tarehe 28 tukapige kura ndio wito wangu, tuwachague viongozi ambao tutaona watatuletea maendeleo, tukawachague na mkuu wa mkoa anasema yule ambaye anaona hajakaa sawa kiroho akaenda kimwili tutamrudisha, mrudisheni kikwelikweli, asituvunjie amani yetu, mrudisheni, awe katika mstari barabara, tukapige kura asubuhi tumchague kiongozi tunayemtaka, kisha baada yah apo turudini kwenye makazi yetu,” Alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Rukwa, mh. Joachim Wangabo aliyehudhuria katika dua hiyo maalum amesema kuwa kuna matayarisho ya kimwili na kiroho katika kuliendea zoezi la uchaguzi mkuu na kuongeza kuwa matayarisho ya kimwili yote yamekamilika ikiwemo Tume ya uchaguzi ya Taifa Pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kujipanga vyema kukabiliana na wale ambao watakuwa wamekengeuka ambao hawataki kufuata maswala hayo ya kimwili.

“ lakini tupo hapa kuwaombea hao na kuiombea nchi yetu amani, sina shaka kabisa, Mwenyezi mungu amekuwa akitusikia, Ametusikia kwenye janga lile la Corona, sasa na hili pia atatusikia, imeandikwa kwenye maandiko matakatifu kwamba wakutanapo wawili wakimuomba yeye yupo na hapa tupo Zaidi ya wawili, tuko wengi viongozi hawa waliopo hap ani wawakili tu wa waumini wote,” Alisema.

 Maombi hayo yalifanyika jana (26.10.2020) katika viwanja vya Shule ya Sekondari kizwite ikiwa ni kutimiza azma ya Kamati ya Amani mkoa kuliombea taifa kuwa na uchaguzi wa amani

 

MWISHO

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.