Na. Revocatus Kassimba,
Wizara ya Kilimo imesaini mkataba wa makubaliano
na taasisi ya BRITEN kuhusu kuendeleza sekta ya kilimo kwa kufanya kilimo
biashara na kuongeza upatikanaji wa pembejeo na masoko kwa wakulima.
Makubaliano hayo yanahusisha kuimarisha ujuzi wa
biashara kwa wakulima wadogo ili kufanya kilimo biashara na kuimarisha uwezo wa
kutunza mazao kabla na baada ya mavuno ili kupunguza upotevu.
Mkataba huo wa makubaliano umesainiwa leo (30.09.2020)
baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya na Afisa Mtendaji Mkuu wa
Building Rural Incomes Through Entrepreneurship (BRITEN) Josephine Kaiza jijini
Dodoma.
Akizungumza wakati wa utiaji saini Kusaya alisema
mkataba huo utasaidia wizara kutumia fursa ya kuongeza ujuzi wa wakulima
kufanya kilimo biashara, matumizi ya teknolojia na kuwapatia mbinu bora za kuongeza kipato.
![]() |
Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya ( wa tatu toka kulia) na watendaji wa shirika la BRITEN mara baada ya kusaini mkataba wa makubaliano leo jijini Dodoma |
“Tunataka kupitia ushirikiano huu na BRITEN
tuwasaidie wakulima hususan wadogo kuongeza kipato, usalama wa chakula ili
sekta ikue zaidi na kuongeza tija na pato la taifa” alisisitiza Kusaya
Eneo jingine la ushirikiano ni kutoa huduma za
upatikanaji habari, pembejeo na kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa wakulima
wadogo wadogo kutumia tafiti na uvumbuzi wa teknolojia mpya za kilimo.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Kusaya alieleza
mkakati wa wizara kuhakikisha inapima sampuli za udongo katika wilaya zote
nchini ili kuwasaidia wakulima na wawekezaji kujua virutubishi gani na aina ipi
ya mbolea au zao la kupanda.
Alisema tayari kituo cha utafiti wa kilimo (TARI)
Selian cha Arusha kimekusanya sampuli za udongo toka kata zote 3,956 za
Tanzania bara ili kujua aina gani ya zao inastahili wapi na mbolea gani ya
kutumia ili kuwa na uhakika na kilimo.
“Tunahitaji tabia za udongo ziwe wazi na kuwezesha
wakulima na wawekezaji kujua eneo la kwenda kulima na aina gani ya zao na
pembejeo za kutumia’ alisema Katibu Mkuu huyo.
Ili kutekeleza mkataba huo wa makubaliano, Katibu
Mkuu Kusaya ameelekeza iundwe kamati ndogo ya watalaam wa wizara itakayofanya
kazi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mkataba uliosainiwa na mingine ya aina
hiyo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRITEN
Josephine Kaiza alisema shirika lao limebobea katika kutekeleza miradi ya
kilimo kibiashara na kutengeneza ushindani wa kibiashara kwa kuwafundisha
wakulima mbinu za uzalishaji bora wa mazao.
Josephine alitaja mafanikio ya taasisi hiyo kuwa
imewafanikiwa kuongeza muunganiko wa wadau wa sekta ya kilimo kufanya kazi kwa
pamoja na kugusa maisha ya wakulima 165,000 mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
“Tunaamini kupitia makubaliano haya tutaweza
kuchangia maendeleo ya kilimo kwa ufanisi zaidi na kufikia wakulima wengi zaidi“
alisema Josephine.
Taasisi ya BRITEN imekuwa ikitekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo ya kilimo kwa takribani miaka 10 na kupitia makubaliano
na wizara ya kilimo wataendelea kutekeleza mpango mkakati wa pili wa ukuzaji
sekta ya kilimo nchini (ASDP II).
Mwisho
Comments
Post a Comment