NGARA WASISITIZWA KUTUNZA MIRADI YA KIJAMII

 Veronica Simba – Ngara

Serikali imewaasa wananchi wa Ngara, Mkoa wa Kagera kutunza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijamii, inayoendelea kutekelezwa wilayani humo kupitia Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera (megawati 80).

Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi wa Umeme wa Rusumo unaotekelezwa wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, Mhandisi Costa Rubagumya (kushoto), akizungumza jambo wakati wa ziara ya Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo, Septemba 29, 2020. Hapa ni Shule ya Sekondari Bukiriro ambayo ni mnufaika wa Mradi huo. Kulia ni Mjumbe wa Bodi ya Mradi huo, Mhandisi Innocent Luoga na katikati ni Gaspar Mashingia, Afisa Mwandamizi, Jamii, Maendeleo na Uhamaji Makazi


Wito huo ulitolewa jana Septemba 29, 2020 na Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo ikihusisha Wakurugenzi wa Bodi na Kamati ya Ufundi, wakiwa katika ziara ya kazi yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi husika.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na Maafisa Watendaji pamoja na wananchi katika maeneo mbalimbali kulipo na miradi hiyo, Kiongozi wa Timu hiyo, Mhandisi Innocent Luoga ambaye ni Mjumbe wa Bodi wa Kamati husika, alisema endapo miundombinu hiyo ya miradi husika isipotunzwa, itakuwa ni hasara kwa Serikali na wananchi walengwa.

“Miradi hii inayohusisha shule, vituo vya afya, miradi ya maji, miundombinu ya kilimo na ufugaji bora inalenga kuwanufaisha wananchi, hivyo ili lengo hilo litimie, inabidi itunzwe.”

Timu hiyo ikiwa katika siku ya pili ya ziara yake, ilitembelea miradi kadhaa ikiwemo Shule ya Msingi Makugwa iliyopo katika kijiji cha Mukubu ambayo imenufaika na Mradi huo kwa kujengewa vyumba vya madarasa, Ofisi na nyumba za walimu, vyoo vya wanafunzi pamoja na tanki la maji safi.

Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi wa Umeme wa Rusumo unaotekelezwa wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, Mhandisi Costa Rubagumya (kushoto), akizungumza jambo wakati wa ziara ya Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo, Septemba 29, 2020. Hapa ni Shule ya Sekondari Bukiriro ambayo ni mnufaika wa Mradi huo. Kulia ni Mjumbe wa Bodi ya Mradi huo, Mhandisi Innocent Luoga na katikati ni Gaspar Mashingia, Afisa Mwandamizi, Jamii, Maendeleo na Uhamaji Makazi


Mwalimu Siyajali Manyasi ambaye ni Mkuu wa Shule hiyo aliueleza Ujumbe huo wa Serikali kuwa, kujengwa kwa miundombinu hiyo kumeiwezesha Shule hiyo kupata usajili na kujitegemea kutoka kuwa tawi la Shule ya Msingi Mukubu iliyoko umbali mrefu kutoka hapo.

“Uwepo wa Shule hii umewapunguzia watoto adha ya kutembea mwendo mrefu takribani kilomita 10 kwenda Mukubu na pia uwepo wa majengo haya ya kisasa umevutia wazazi wengi zaidi kuwaleta watoto wao shuleni,” alisema Mwalimu Manyasi.

Vilevile, Timu hiyo ilitembelea Shule ya Sekondari Bukiriro ambayo imenufaika kwa kujengewa bweni la wanafunzi wa kike, bwalo la chakula na vyoo.

Aidha, Ujumbe huo ulitembelea Chuo cha Ufundi Stadi Lemera kilichopo katika kijiji cha Mukibogoye kilichonufaika kwa kujengewa karakana ya useremala na ushonaji nguo pamoja na uwanja wa michezo ambao ujenzi wake unaendelea.

Timu ilitembelea pia miradi ya kilimo cha kisasa kwa njia ya banda kitalu maarufu kama ‘green house’ kwa lugha ya kigeni na mradi wa ufugaji nyuki, inayotekelezwa katika kijiji cha Chivu, Kata ya Ntobeye, yote ikilenga kuwanufaisha wananchi kiuchumi.

Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikizungumza na wanafunzi katika Shule ya Msingi Makugwa iliyopo katika kijiji cha Mukubu, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo Septemba 29, 2020 ambapo Shule hiyo imenufaika kwa kujengewa vyumba vya madarasa, nyumba na ofisi za walimu, tanki la maji savi na vyoo vya wanafunzi


Akizungumza katika ziara hiyo, Mratibu wa Miradi ya Maendeleo ngazi ya Wilaya, Herman Hume alieleza kuwa miradi hiyo ya kijamii inayoendelea kutekelezwa wilayani Ngara ilitengewa fedha kiasi cha dola milioni tano za Marekani ambazo ni sawa na takribani shilingi bilioni 12 za Tanzania.

Kwa upande wao, Mhandisi Salum Inegeja kutoka Wizara ya Nishati na Mhandisi Costa Rubagumya kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi wa Rusumo, walikiri kurudhishwa na utekelezwaji wa miradi hiyo lakini wakasisitiza umuhimu wa kuifanya iwe endelevu kwa maslahi ya wananchi.

Katika ziara hiyo, Timu ilifuatana pia na Mhandisi Patrick Lwesya, Meneja Mradi wa Rusumo, Gaspar Mashingia, Afisa Mwandamizi, Jamii, Maendeleo na Uhamaji Makazi pamoja na Maafisa kadhaa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.

Mradi wa Umeme Rusumo unatekelezwa kwa ushirikiano wa nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi ambapo utakapokamilika unatarajiwa kuzalisha megawati 80 za umeme zitakazogawanywa kwa nchi husika.

 

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.