WANANCHI WASHAURIWA KUWAPIGIA KURA VIONGOZI WATAKAO LETA MAENDELEO

 

CHAMWINO,DODOMA.

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la AFNET Sara Mwaga,amewaomba wananchi wa kijiji cha Kawawa wilaya ya Chamwino ambao wana vitambulisho vya kupiga kura kuvitendea haki kwa kuwapigia viongozi watakaoleta maendeleo kwa masilahi ya watanzania wote.

Aidha amewahamasisha wananchi hao kuhakikisha hawapotezi haki yao kutokana na kudanganyika kwa kununuliwa chakula,vitenge,fedha na kanga,kwa kuwa wanaweza kujikuta ikiwagharimu kwa kuwachagua viongozi mabomu wenye kujali maslahi yao.

Mwaga alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji hao walioshiriki kwenye maombi maalumu kuombea Taifa na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu yaliyoandaliwa na kanisa la Kipentekost la Sayuni Tanzania lililopo kijiji cha Kawawa kata ya Msanga wilayani Chamwino.

Alisema wananchi wenye vitambulisho hivyo vya kupiga kura wanatakiwa kutumia haki ya kimsingi ya kuwachagua viongozi watakaofanisha kutatua changamoto za watanzania bila kujali watu watakaowatumikia wanatoka kwenye chama kipi.

Mkurugenzi huyo amewaomba wananchi hao walioshiriki kwenye maombi hayo ambao wana vitambulisho vya kupigia kura kuacha tabia ya kubweteka majumbani siku ya upigaji,badala yake wajitokeza watumie haki ya msingi ya kuwapata viongozi wanaowataka wao wenyewe.

“Haipendezi mwananchi una kitambulisho cha mpiga kura halfu ukakaanacho nyumbani siku ya upigaji kura,ninawaomba mjitokeze kwa wingi ili mtumie haki yenu ya kisingi ya kuwachagua viongozi mnaowataka wenyewe na msisubiri kuchaguliwa na wengine”alisema.

Kwa upande wake Mchungaji kiongozi Jonas Kabia wa kanisa hilo la Sayuni,alisema kuwa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu Taifa la Tanzania halitegemei kuwapata viongozi watakaowagawa watanzania kutokana na itikadi za vyama vyao.

Alisema watanzania mategemeo yao makubwa  kwenye uchaguzi huu wa mwaka 2020 ni kuona wanatumia demokrasia ya haki na huru katika kuwachagua viongozi wanaowania nafasi hizo ikiwemo ya urais,ubunge na udiwani.

Hata hivyo alisema kuwa malengo ya maombi hayo maalumu ni pamoja kumumba Mungu ili awawezeshe viongozi watakaochaguliwa kwenye uchaguzi huu wa 2020 waweze kutekeleza ahadi ambazo watakazozisema kupitia sera za vyama vyao.

MWISHO.

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.