Na. Revocatus Kassimba, MANYARA
Serikali
imeviagiza viwanda vya mbolea nchini kuzalisha mbolea yenye viwango vya juu vya
ubora na kuiuza kwa wakulima kwa gharama nafuu ili uzalishaji wa mazao uwe na
tija na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya ametoa kauli hiyo leo (28.08.2020) mkoani Manyara alipotembelea kukagua kiwanda cha mbolea cha Minjingu.
Alisema
ameamua kufanya ziara kwenye mikoa iliyo na viwanda vya mbolea ili kuona namna wanavyozalisha
ili kukidhi upungufu mkubwa wa mbolea ndani ya nchi hali inayopelekea wakulima
kununua kwa bei kubwa.
“Nimeamua
kufanya ziara hii kutembelea viwanda vya mbolea na kuongea na wazalishaji ili
kuhamasisha upatikanaji wa mbolea yenye virutubisho bora na itakayouzwa kwa bei
nafuu kwa wakulima nchini” alisema Kusaya.
Kusaya
aliongeza kusema katika ziara zake nyingi mikoani alipokea malalamiko ya
wakulima kuuziwa mbolea kwa bei kubwa na kutolea mfano mkoa wa Kagera alikuta
mfuko wa kilo hamsini wa DAP ukiuzwa kati ya shilingi 80,000 hadi 90,000 kutokana
na mbolea hiyo kuagizwa nje ya nchi.
“Lengo
la serikali ni kumkomboa mkulima, lakini hatuwezi kufikia lengo hilo kama
mbolea itaendelea kuuzwa kwa bei kubwa nchini.Ndio maana Tunataka viwanda vijengwe
hapa nchini “ Kusaya alisema.
Katibu
Mkuu huyo alisema mahitaji ya mbolea nchini ni takribani tani 664,000 wakati
uzalishaji kwenye viwanda vyote 12 umefikia tani 38,000 pekee kwa mwaka.
Akizungumza
kuhusu changamoto za kiwanda cha mbolea Minjingu kuwa na uzalishaji mdogo, Meneja
Masoko wake Franks Kamhabwa alitaja tatizo la upatikanaji soko kukwamisha
uzalishaji zaidi.
Kiwanda
cha mbolea cha Minjingu kina uwezo wa kuzalisha tani 100,000 za mbolea kwa
mwaka kutokana na akiba ya madini ya Phosphate takribani tani milioni 8 hadi 10
kwenye mgodi wake lakini sasa hivi wanazalisha tani 23,598 kwa mwaka.
Kamhabwa alitoa ombi kwa serikali kuwa kiwanda cha mbolea Minjingu kipewe fursa ya kupata soko la ndani ya nchi kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Pamoja (BPS) sawa na mbolea zinazoagizwa nje ya nchi.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Minjingu Tosky Hans aliishukuru serikali kwa
kukiunga mkono kiwanda hicho hali inayojidhihirisha kupitia Viongozi mbalimbali
kuizungumzia vizuri mbolea ya Minjingu.
“Kiwanda
hiki kilikuwa yatima huko nyuma, tunashukuru serikali ya Awamu ya Tano imetushika
mkono kutusaidia bidhaa zetu sasa zinakubalika sokoni “alisema Hans.
Hans
alimweleza Katibu Mkuu huyo wa Kilimo kuwa malengo ya kiwanda cha Minjingu ni
kufikia uzalishaji wa tani 500,000 ifikapo mwaka 2025 na kuwa wataanzisha
mashamba ya majaribio (Demo plots) katika halmashauri mbalimbali ili zitumike
kufundishia wakulima juu ubora wa mbolea ya Minjingu.
Katika
hatua nyingine Kusaya alitembelea viwanda vya kuzalisha mbolea za maji (Boosters)
vya Kahela Feeders na Keen Feeders Ltd vya Arusha na kujionea hali ya
uzalishaji bidhaa hiyo.
Akiwa
katika kiwanda za mbolea Keen Feeders kilichopo Ngaramtoni Arusha alifahamishwa
kuwa kiwanda hicho huzalisha lita 600,000 za mbolea ya maji na kuuzwa kwa
wakulima hali inayosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao.
Mkurugenzi
Mkuu wa kiwanda hicho cha Keen Feeders Alfred Masawe alisema wanakutana na
changamoto ya upatikanaji wa vifungashio na mitaji hali inayopelekea bei ya
mbolea hiyo kuwa juu.
Katibu
Mkuu Kusaya akiwa kwenye viwanda hivyo alibaini kuwepo kwa mapungufu ya bidhaa
zinazozalishwa kutokuwa na nembo ya usajili wa ubora kutoka Shirika la Viwango
Tanzania (TBS)
Kusaya
ameagiza wamiliki wa viwanda vyote ambavyo havina usajili wa Shirika la Viwango
(TBS) pamoja na mamlaka zingine za udhibiti kwenda kuomba leseni hizo ili wawe na uhakika
wa soko na kulinda mazao ya wakulima na binadamu watakaotumia mazao
yaliyozalishwa kwa mbolea hiyo aina ya Booster.
Kuhusu
changamoto ya mitaji kwa wazalishaji wa mbolea za Booster ,Kusaya amewataka
waende Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Mfuko wa Pembejeo nchini ( AGTIF)
kukopa kwa kuwa ni taasisi za serikali na zinatoa riba nafuu kwa wakulima na
wananchi.
“Nendeni
TADB na AGTIF kukopa mitaji ya kukuza uzalishaji wa mbolea kwenye viwanda vyenu
ili wakulima wapate mbolea hizo kwa gharama nafuu zaidi” alisema Kusaya.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA)
Dkt. Stephano Ngailo aliyeambatana na Katibu Mkuu kwenye ziara hiyo amemshukuru
kwa kazi kubwa aliyoifanya kutembelea na kuhamasisha wazalishaji mbolea kwenye
mikoa mitano.
Dkt.
Ngailo alisema amepokea malekezo yote ya serikali yaliyotolewa na Katibu Mkuu
na kuwa watahakikisha wazalishaji wa mbolea nchini kote wanazingatia ubora na
kuuza bidhaa hizo kwa gharama nafuu ili iwafikie wakulima wengi.
Kusaya
pia ameagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) kufanya ukaguzi wa mbolea
zisizo na viwango (fake) ambazo zinalalamikiwa na wazalishaji wadogo kuwa
zinaharibu soko lao kwa kuuzwa mitaani.
“
TFRA fuatilieni mbolea (booster) zisizo na ubora kwenye masoko ya Kariakoo, Arusha,
na kwingineko mikoani na kuchukua hatua
kali za kisheria kwa wauzaji na watengenezaji ili kudhibiti zisiendelee kusambaa.Nipate taarifa yenu ya
utekelezaji mapema.” aliagiza Katibu Mkuu Kusaya akiwa Arusha.
Katibu
Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo amehitimisha ziara yake ya kutembelea viwanda vya
mbolea na kukutana na wazalishaji katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga,
Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambapo imemwezesha kujionea hali halisi ya
uzalishaji na upatikanaji mbolea nchini.
Mwisho.
Comments
Post a Comment