Umoja wa waalimu wa Hedhi Salama kwa shule za msingi mkoani Rukwa wamepania kuhakikisha wanapunguza fikra potofu kuhusu suala la hedhi kwa wasichana wanaovunja ungo pamoja na kukomesha utoro kwa wananfunzi wa kike wanaoona aibu kuhudhuria shule pindi wanapopata hedhi kwa kutoa elimu sahihi ya suala la hedhi mashuleni.
Azma hiyo imekuja baada
ya waalimu hao kupewa mafunzo yanayohusu namna ya kutengeneza pedi kwa kutumia
aina mbalimbali za vitambaa pamoja na kukabiliana na wanafunzi wanaoona aibu
ama fedheha pindi wanapopata hedhi wakiwa shuleni na hivyo kuwarahisishia
Maisha yao wanapokuwa shuleni huku wakiwahamasisha kuendelea kuhudhuria shuleni
ili wasiachwe nyuma kimasomo.
Aidha Mwanauta ni
mwalimu wa Hedhi Salama kutoka Shule ya Msingi Ilambila, Wilayani Kalambo,
aliishukuru serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo muhimu kwani changamoto
wanazokumbana nazo ni nyingi na mafunzo hayo yamamsaidia kujua namna ya
kuwasaidia wasichana hao pindi wanapokuwa katika hedhi kutokana na wanafunzi
wengi kutokuwa na ufahamu wa kutosha juu ya namna ya kukabilina na hali hiyo.
“Kuna mwanafunzi anakuja
shuleni hajui ni namna gani anaweza akajistiri, mwingine anatoka nje anakimbia,
huko nje anachukua hata makaratasi, majani kwaajili ya kujistiri ambayo inaweza
ikamletea matatizo baadaye, kwahiyo katika semina hii tumejifunza mambo
mbalimbali, tumejua ni mambo gani ambayo unaweza ukamfundisha mtoto, akajua
jinsi ya kujihifadhi akiwa shuleni na hatimae akawa anasoma na asiwe mtoro
shuleni, na kujiona ni sawa na wengine,” Alisema.
Nae, Mwalimu Victoria
Tanganyika alisema kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kujua vifaa vinavyotumika
kutengeneza pedi za kike na namna ya kuvitekeza pamoja na kujua mazungumzo
anayotakiwa kufanya na matoto ili kumshawishi aweze kujiamini na
kushiriki katika michezo na masomo katika mazingira ya shule.
Kwa upande wake Mwalimu
Clifonsia Remidio ameiomba serikali kuendelea kutumia njia mbalimbali za
vipeperushi na kutoa semina kwa waalimu wengi zaidi wanaotoa huduma ya hedhi
salama mashuleni ili kuweza kuwasaidia wanafunzi wa kike ambao wamekuwa
wakipata tabu kusoma wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.
“kuna vitu vingi
tulikuwa hatuvifahamu, kuna wakati mwingine hata kama mimi mwalimu nimeshasoma
lakini bado nitaona aibu kuenenda kumuelekeza yule mwanafunzi, lakini
ameshatuelekeza mwezeshaji tumepata mwanga mzuri pia nimefurahi kwasababu hili
suala linashirikisha pande zote mbili, upande wa waalimu wa kiume na upande wa
waalimu wa kike pia kwamba tuwasaidie Watoto wanaposikia ile hali ya mabadiliko
ya mwili,”Alisema.
Aidha, Mwezeshaji wa
mafunzo hayo ya Hedhi Salama, Mwalimu Jesca Lwiza alisema kuwa mafunzo hayo
yanalenga kutoa elimu ya hedhi salama kwa wanafunzi ili kupunguza utoro
mashuleni na kuongeza kuwa wanategemea kuona mabadiliko makubwa ya mahudhurio
shule kwa shule ambazo waalimu wake wamehudhuria mafunzo hayo.
“Kuna ukimya ambao upo
katika masuala ya hedhi salama, wanafunzi wanakosa elimu sahihi, lakini pia
wanakosa namna ya kujiamini wanapokuwa katika masomo na wakati mwingine shuleni
hakuna vyumba maalum vya kujihifadhi wanapokuwa katika hedhi, kwa kulitambua
hilo tumeona serikali namna ilivyoweza kuwezesha kwa kuwapa mafunzo waalimu
lakini imeweza kuboresha miundombinu iliyopo mashuleni kwa kuweka vyumba
hivyo,” Alisema.
Wakati akifungua mafunzo
hayo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi alisisitiza kuwa tafiti
zilizofanyika zimeonesha kuwa wasichana wengi hawana taarifa za awali kuhusu
hedhi za pia walipata hedhi ya kwanza pasipo kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu
mabadiliko ya miili yao hivyo mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waalimu
kufikisha elimu katika shule.
“Tafiti zinaonesha kuwa
bado kuna fikra zisizo sahihi kuhusu masuala ya hedhi hususani miiko na
unyanyapaa inayosababisha wasichana na wanawake kushindwa kushiriki kikamilifu
katika shughuli za maendeleo na kijamii na wanafunzi wa kike kukosa baadhi ya
siku za masomo na wengine kuacha shule wanapokuwa kwenye hedhi. Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kulitambua hilo imeweka jitihada
kuhakikisha kuwa fursa za elimu zinapatikana kwa makundi yote,” Alieleza.
Halikadhalika mratibu wa
mradi wa School Water Sanitation and Hygiene (SWASH) Mwalimu Matinda Mwinuka
aliwaasa waalimu kuhakikisha shule zinakuwa na vyombo maalum kwaajili ya
walemavu pamoja na vyumba kwaajili ya wasichana kubadili pedi za hedhi pindi
wanapokuwa katika hali hiyo nasio kutumia vyoo vya kawaida ambavyo havina mazingira
mazuri ya kubadilishia vifaa vyao.
“Kuna shule moja fundi
kaweka shule maalum, anasema kuwa kile ndio chumba maalum, walemavu wataingia
humo humo, hedhi salama wataingia humo humo, ametoboa tundu na kuweka ‘pipe’
anasema Watoto wa kike wakishaingia humu ndimo watatumbukiza vile vitu vyao
yaani ni vitu vya ajabu kwakweli.”
Mradi huo unatekelezwa
katika halmashauri tatu za Mkoa wa Rukwa kwa muda wa miaka minne huku kwa mwaka
wa fedha 2019/2020 Mkoa ulipewa kiasi cha Shilingi 578,486,955.63/= kwaajili ya
utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kutekelezwa katika
mikoa 17 na Halmashauri 86 za Tanzania Bara ukiwa na lengo la kuboresha
mazingira ya kufundishia, kujenga vyoo bora shuleni na kuweka miundombinu ya
maji safi na salama.
MWISHO.
Comments
Post a Comment