Wanafunzi Shule ya Msingi Dodoma Mlimani waeleza Furaha yao Baada ya kurejea Shuleni,Tutasoma kwa Bidii,Tuliwakumbuka sana Walimu wetu, Muda wa kucheza haupo tena

Wanafunzi wa Darasa la saba  wa Shule ya Msingi Dodoma Mlimani  wakinyoosha mikono kwaajili ya kujibu maswali yaliyokuwa yakiulizwa na Mwalimu aliyekuwa akiwafundisha Darasani



Na Jackline Kuwanda, Dodoma.

Wanafunzi wa shule ya Msingi Dodoma Mlimani iliyopo Mkoani Dodoma wameonesha hali ya furaha kwa kurejea tena shuleni baada ya kukaa nyumbani kwa takribani miezi mitatu kutokana na Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19).

Janga la Corona lilichangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha kuendelea kwa shughuli mbalimbali hapa Nchini ikiwemo pia Vyuo kufungwa, Shule za Awali ,Msingi na Sekondari nazo zilifunguwa lengo lilikuwa ni kuepusha kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huu.

Jumanne June 16,2020 wakati akitoa hotuba yake ya kuvunja Bunge la 11, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli alitangaza rasmi kufunguliwa kwa shule zote zilizofungwa kutokana na ugonjwa huo na June 29 ndiyo ilikuwa tarehe rasmi ya wanafunzi kurejea shuleni.


Dodoma News Blog ilitembelea shule hiyo ili  kujionesha hali halisi baada ya wanafunzi pamoja na walimu kurejea shuleni .

‘’Tuliwakumbuka sana walimu wetu kipindi tulichokuwa nyumbani,muda mwingi umepotea, kwa sasa tumerejea shuleni  sio muda wa kucheza tena, tutasoma kwa bidii na tutafaulu’’


Wanafunzi wa Darasa la Saba katika shule hiyo ambao wanatarajia kufanya mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi hivi karibuni wanaeleza namna ilivyokuwa kipindi walipokuwa nyumani na sasa wamerejea shuleni .

Hemedy shabani ambaye anasoma Darasa la saba katika shule hiyo alisema anafuraha sana kurejea shuleni lakini katika kipindi chote alichokuwa nyumbani alikuwa akijisomea kwenye madaftari yake lakini pia kupitia Runinga.

‘’najua kuwa ninatarajia kufanya mtihani wangu wa kuhitumu elimu ya msingi nitasoma kwa bidii kwakuwa muda tuliyopoteza ni mwingi sana sasa hivi sio muda wa kucheza’’ Alisema Hemed

Grace Steven alisema wakati yuko nyumbani alikuwa akijifunza masomo ya Darasa la saba kupitia Radio  kwani alikuwa akijitahidi kusikiliza kwa umakini na alikuwa akiwaelewa walimu ambao walikuwa wakifundisha.

‘’kazi walizokuwa wakitupa nilikuwa nafanya na majaribi mengine nilikuwa nafanya kupitia mitihani yangu ya zamani niliwakumbuka walimu wangu jinsi walivyokuwa wanatufundisha’’ Alisema Grace

Naye Elizabelth David ambaye pia yuko Darasa la saba alisema amerejea tena shuleni hivyo atasoma kwa bidii ili aweze kufaulu mitihani yake vizuri.

‘’tuliwakumbuka sana walimu wetu,Tumekaa nyumbani muda mrefu na hivi sasa tumerejea shuleni nitasoma kwa bidii,nakumbuka wakati niko nyumbani nilikuwa na muda wa kujisomea kupitia madaftari yangu na kupitia runinga kwenye Darasa huru’’ Alisema Elizabelth

Nao wanafunzi wa Darasa la nne katika shule hiyo walisema kuwa wanajisikia vizuri kurejea tena shuleni na wamejipanga vyema katika masomo huku wengine wakisema kuwa walikaa nyumbani ili kuepuka kuenea kwa janga la corona na sasa wamerejea shule watasoma kwa bidii na watafaulu.
Mwalimu Abubakari Shabani wa Shule ya Msingi Dodoma Mlimani anayefundisha Masomo ya Sayansi na Kingereza Darasa la saba katika shule hiyo



Mwalimu Abubakari Shaban ni mwalimu wa Darasa la Saba kwa somo la sayansi na kingereza yeye alisema kuwa wamejipanga vizuri katika kufuata miongozo mbalimbali iliyotolewa ikiwemo kuongeza muda wa masomo.

‘’kwenye kuongeza muda wa mosomo na vipindi viteongezeka na sisi tutaenda kwa kasi ili kuziba lile gepu ,na tutajitahidi kwenda kwa kasi ili kufanya wanafunzi waweze kuelewa ili kwa yale madara ya mitihani waendelee kujiandaa vizuri na mitihani yao ‘’Alisema Shaban

‘’Mikusanyiko ilikataliwa kama unavyojua ufundishaji wetu wanafunzi ni lazima waje shueleni sasa baada ya kufunga ikawa kuwapata wanafunzi ni changamoto kubwa,licha ya kuwa kuna vipindi vilikuwa redioni na kwenye Runinga ilikuwa bado ni changamoto kwa zile familia ambazo hazina uwezo huo ’’ Alisema Shaban
Mwalimu Happines Sumaye anayefundisha Darasa la Nne katika shule hiyo akielezea furaha yake baada ya kurejea Shuleni


Kwa upande wake Mwalimu Happines Sumaye anayefundisha Darasa la nne katika shule hiyo amesema anajisikia furaha kwa kurejea shuleni kwasababu ni kazi ambayo wanaipenda.

‘’tunapenda kuona jamii iliyo elimika , iliyostaarabika kwa hiyo kwa kipindi ambacho hatukuwa shuleni kutokana na janga hili,tuliokuwa tunaona kabisa taifa letu linavyokwenda kuporomoka lakini tunamshukuru Mungu hali imerejea kuwa nzuri, watoto wamerejea shuleni wote wana afya nzuri ,tunamshukuru Mungu tunaendelea na kazi’’ Alisema Sumaye

Dodoma News Blog ilizungumzana  Mwalimu Mkuu wa Shule Teonila Mgulunde alisema anafurahi sana kufunguliwa kwa shule kwani kwa kipindi cha miezi mitatu wanafunzi kukosa masomo ni ngumu mno na imewaumiza kwa kiasi kikubwa.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Dodoma Mlimani Teonila Mgulunde


‘’Tunaishukukuru sana serikali kwa uamuzi wake huu ,kwani idadi ya watoto waliorudi shuleni ni wengi licha ya kuwa kuna mmoja tumempoteza lakini hakuuumwa ugonjwa huu alikuwa na matatizo mengine lakini anamini kuwa baada ya kurejea shuleni malengo yatatimia kwasababu tumeongezewa masaa ya vipindi kuzalishwa vipindi katika masaa mawili ndivyo tulivyoambiwa kwenye muongozi ambao ulitolewa’’ Alisema Mgulunde

Akizungumzia kwa Madara ya mitihani alisema kuwa masaa mawili ambayo yaliongezwa yanawahusu kama kawaida kwani katika shule yao wameshamaliza mada tangu mwezi wa tatu.

‘’kwahiyo tuko katika marudio watoto wataendelea kufanya mitihani siku ya jumatano na siku ya jumamosi na tutafanya tathimini mtihani wa jumamosi kwahiyo tukishafanya tathimini lazima jumatano tufanyishe tena mtihani mwingine mpaka siku ya mtihani wa Taifa hapo ni kwa darasa la saba lakini kwa upande wa Darasa la nne wataendela kufanya mtihani siku ya jumamosi’’ Alisema Mgulunde

Hatahivyo alisema kutokana muda wa vipindi kuongezwa amewasihi wazazi kuhakikisha kuwa mtoto anapotoka nyumbani anakula vizuri lakini kwa wanaohitajika kuvaa barakoa wazazi pia wanapaswa kuwahimiza watoto kuvaa barakoa kwani wapo watoto ambao hawai kutokana na sababu za kiafya.

Tanzania ni Miongoni mwa nchi chache ambazo zimefungua milango kwa wanafunzi kurudi shule baada ya serikali kujiridhisha kupungua kwa maambukizi ya Covid-19 huku ikisisitiza tahadhari kuendelea kuchukuliwa.

Mwisho.


Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.