YALIYOJIRI LEO MEI 30, 2020 WAKATI RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. JOHN POMBE MAGUFULI AKIWAKABIDHI NDEGE AINA YA TAUSI MARAIS WASTAAFU PAMOJA NA KUWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA OFISI ZA IKULU CHAMWINO, DODOMA




HAFLA YA MAKABIDHIANO YA NDEGE AINA YA TAUS*

#Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipoingia madarakani alikuta ndege aina ya tausi 403, hadi sasa wameongezeka na kufikia 2260. Tausi hao pia wamepelekwa katika Ikulu za mikoani, takriban tausi 540 wako katika Ikulu ya Dodoma.

#Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewakabidhi kila mmoja Hati na ndege 25 aina ya Tausi kwa Mjane wa Hayati Baba wa Taifa pamoja na Marais Wastaafu watatu.

#Ugawaji wa ndege hawa kwa Mjane wa Hayati Baba wa Taifa na Marais Wastaafu ni tukio kubwa na la kwanza hivyo napendekeza itokee siku na wewe uridhie ili tukukabidhi na wewe Rais Dkt. Magufuli ndege hawa kabla ya kustaafu - Katibu Kiongozi, Balozi John Kijazi.

#Tukio hili linaashiria kuwa pamoja na viongozi kustaafu lakini bado mpo pamoja na Serikali - Balozi, John Kijazi.

#Nawashkuru Marais Wastaafu kwa kukubali kuja kuchukua ndege hawa. Ndege hawa wana historia, Tanzania hatukuwahi kuwa na Tausi bali waliletwa na Hayati Baba wa Taifa katika kipindi cha utawala wake lakini wametunzwa vizuri na Marais Wataafu - Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

#Hayati Baba wa Taifa aliwapenda hawa ndege hivyo nimeona nitoe ndege hawa wakakae Butiama hata watu wanaoenda kutalii pale wakafahamu kuwa haya ni matokeo ya upendo na busara yake kwa Watanzania, pia wazee hawa waliwapenda na kuwatunza ndege vizuri ndio maana nimefanya uamuzi huo - Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

#Nakushkuru umefanya jambo kubwa kwa ajili yetu, tumefurahi sana pia nakupongeza kwa maendeleo makubwa yanaondelea hapa katika Ikulu hii - Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.


HAFLA YA UWEKAJI JIWE LA MSINGI UJENZI WA OFISI ZA IKULU CHAMWINO DODOMA

#Eneo la Ikulu ya Dodoma lina zaidi ya hekari 8473 ambapo limezungushiwa ukuta wenye urefu wa KM 27. Kwa ukubwa wa eneo hili linaifanya Ikulu ya Tanzania kuwa ni moja ya Ikulu kubwa Duniani.

#Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameendelea kuweka wanyama mbalimbali katika Ikulu hii ambapo kwa kasi hii ya kuongezeka kwa wanyama yapo mawazo ya kupafanya pawe na hifadhi ya wanyama ili watalii waje kutembelea na kuongeza pato katika nchi yetu.

*Aliyosema Rais DKt. John Pombe Magufuli*

#Kutokana na umuhimu wa jengo hili la Ikulu, sikuona umuhimu wa kufanya jambo hili peke yangu ndio maana nikawaomba Marais Wastaafu tuje tushirikiane pamoja kuweka jiwe hili la msingi.

#Mnamo Oktoba 10,1973 Hayati Baba wa Taifa alitangaza uamuzi wake wa kuhamishia Ikulu jijini Dodoma lakini pamoja na kujengwa kwa makazi ya Rais nilipoingia madarakani niliahidi kuhakikisha Serikali inahamia Dodoma.

#Pamoja na ujenzi unaoendelea, tayari majengo matatu ya awali na ujenzi wa ukuta unaozunguka Ikulu vimeshakamilika. Aidha, hakuna hata jengo moja la zamani litakalobomolewa.

#Nawapongeza jumla ya vijana 2400 waliogawanyika katika makundi mbalimbali pamoja na viongozi wenu kwa kufanya kazi ya ujenzi wa Ikulu hii kwa ubora, endeleeni kuchapa kazi.

#Nimewaagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa jumla ya Sh. Bil. 2 kwa Jeshi la Kujenga Taifa ili kuhakikisha ujenzi wa Ikulu hiyo unakamilika.

#Katika ugonjwa huu wa Corona Mungu ametusaidia tumeshinda, Tanzania tuko salama.

#Ninaomba wakulima tujihadhari na kuuza mazao yetu kwa bei ya chini, mwaka huu umekua mzuri kwani tutapata chakula cha kutosha hivyo kama kuuza tuuze katika muda muafaka, hapo ndipo tutapata faida ya mazao yetu.

#Hivi sasa Dodoma imeshakua, mbali ya kujenga ofisi za Serikali na kufanikiwa kuwahamisha watumishi, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu na kuboresha huduma za jamii.

#Tayari tumejenga barabara nyingi za lami na nyingine zinaendelea kujengwa ikiwemo barabara yenye KM 51 kwenye Mji wa Serikali pia tupo kwenye hatua za mwisho za kumpata Mkandarasi wa kujenga barabara ya mzunguko ya njia nne yenye urefu wa KM 110.

#Tumepanua uwanja wa ndege wa Dodoma, taratibu za kumpata Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mpya mkubwa wa ndege wa msalato mchakato unaendelea.

#Tumekamilisha ujenzi wa stendi kuu ya mabasi kwa gharama ya sh. Bil.24.033 pamoja na soko kuu litakalogharimu sh. Bil.14.649 na kwa upande wa huduma za maji kwa sasa tunaendelea na maandalizi ya ujenzi wa bwawa ambalo litazalisha lita 128,000 kwa siku na umeme upo wa kutosha, kuna ziada ya MW 21 hapa Dodoma.

 *Aliyosema Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.*

#Ningependa kujiunga na wenzangu kutoa pongezi maalum kwa mwenyeji wetu ambaye ni kijana kuliko mimi na ni chanzo chema cha fikra na maendeleo na nina uhakika wote tumefurahi kuona namna anavyoliongoza taifa letu, kwa namna mpya na nzuri. Natoa shuk rani na pongezi za hadharani.

*Aliyosema Rais Mstaafu, Benjamin William Mkapa.*

#Tunashukuru kwa kukumbukwa na kupewa zawadi ya ndege hawa tulio watunza kwa miaka yote 30. Tunakushukuru kwa uaminifu wako kwa Chama na Serikali uliyoiunda. Uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ni jitihada za muda mrefu na kila awamu ilifanya jitihada. Rais Magufuli amefanya mengi zaidi na sasa Serikali imehamia Dodoma. Nasisitiza, Mbele kwa mbele, endelea hivyo! 

*Aliyosema Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.*

#Mwaka 1971 Chama cha Tanu kiliamua Makao Makuu ya Nchi yahamie Dodoma, na ni uamuzi uliofanywa kidemokrasia, Mikoa ilitoa maoni na mingi ilikubali kasoro Mkoa wa Pwani. Ulikua ni uamuzi shirikishi na sio mawazo ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pekee .

#Rais Magufuli nakupongeza sana kwa uamuzi wa busara na wa hekima wa kujenga IKULU, Hapa ndio kilele chenyewe. Naungana na wenzangu kukupongeza na kukuombea uhai ushiriki katika kukata utepe baada ya ujenzi huu kukamilika.

*Aliyosema Katibu Mkuu Ikulu, Moses Kusilo.*

#Mnamo mwaka 2017 shughuli mbalimbali za ujenzi wa majengo mapya, ujenzi wa barabara na ujenzi wa ukuta pamoja na  ukarabati wa majengo yaliyokuwepo.

#Rais Dkt. John Pombe Magufuli mnamo Januari 2020, alielekeza kuanza kwa ujenzi katika eneo hili na kusisitiza kuwa usanifu wa majengo hayo ufanane kabisa na Ikulu ya Dar es Salaam, alisisitiza kuwa ujenzi huo ufanywe na wazalendo wa hapa hapa nchini.

*Aliyosema Mkuu wa JKT, Brigedia Genarali, Charles Mbuge.*

#Jeshi la kujenga Taifa lilikabidhiwa eneo la Chamwino lenye ukubwa wa mita za mraba 9340 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi ya Rais na jengo la utawala mnamo Februari, 2020, ujenzi unaendelea na fedha iliyotolewa hadi sasa ni sh. Bil.1.

#Jeshi la kujenga Taifa limeendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa Corona, tunaendelea kutengeneza barakoa, vitakasa mikono na vifaa kinga na kuviuza kwa wananchi kwa bei rahisi.


IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO


Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.