Vikundi vyashauriwa kujenga uaminifu urejeshaji wa mikopo

Meneja wa Benki ya Nmb Kanda ya Kati ,Nsolo Mlozi (kushoto) akimkabidhi  mfano wa hundi  yenye thamani ya sh milioni 244.6 kwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Eng. Zacharia Chaula (kulia) kwa ajili ya Halmashauri hiyo kukabidhi mikopo kwa baadhi ya vikundi vya Walemavu, Wanawake na Vijana. Benki ya NMB ilikabidhiwa jukumu la kutoa elimu ya kifedha kwa vikundi hivyo kabla ya kupewa mikopo hiyo, wengine katika picha katikati ni mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Simanjiro Yefred Myenzi  (wapili kulia) na makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Sendeu Laizer (wapili kushoto).



Na Mwandishi Wetu,
VIKUNDI vilivyopata mikopo kutoka Halmashauri na taasisi nyingine za kifedha vimeshauriwa kujenga uaminifu katika marejesho ili na wengine waweze kunufaika na fedha hizo.
Hayo yamebainika jana katika hafla ya kukabidhi hundi za mikopo  awamu ya nne  kwa baadhi ya vikundi vya Halmashauri Wilaya ya Simanjiro mkoani  Manyara, jana.
Akizungumza katika hafla hiyo Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi alisema benki hiyo ilikabidhiwa jukumu la kutoa elimu kwa vikundi pamoja na kuwafungulia akaunti jambo ambalo wamelifanya kwa makini na vikundi vyote walifanikiwa kupata fursa hiyo.
“Mbali ya elimu ya fedha, NMB tunashirikiana na halmashauri hii kwa kutoa misaada mingine kwenye jamii hasa sekta  ya elimu, afya na  kwenye majanga mbalimbali,” alisema Mlozi.
Alibainisha, NMB imeendelea kutenga asilimia moja ya faida yake kila mwaka kurudisha kwenye jamii ikiwa ni juhudi za kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli.
Aidha, akitoa taarifa ya mikopo hiyo Mkurungenzi wa Halmashauri ya Simanjiro, Yefred Myenzi alisema jumla ya fedha zilizokopeshwa kwenye vikundi ni zaidi ya Sh Milioni 244.6 kutoka mapato yake ya ndani.
“Walionufaika ni jumla ya wananchi 1412  ndani ya halmashauri hii, ikiwemo wanawake 1074  vijana 372 na walemavua 40. Halmasahuri hii hadi sasa haidawi imeshalipa madeni yote yakiwemo mikopo benki na wakandarasi waliofanyakazi ya eneo hili,” alisema Myenzi.
Alibainisha, fedha hizo zinazotolewa na halmashauri kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu hazina riba wakati wa kurejesha.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Zacharia Chaula alivitaka vikundi vilivyopata fursa ya kupewa mikopo kutoka mfuko wa halmasahuri kuhakikisha wanarejesha kwa wakati ili wengine waweze kufaidika na mikopo hiyo.

Alisema: “lengo la serikali kutoa mikopo hiyo kupitia halmashauri ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi makundi maalumu yaliyoorodheshwa kisheria katika mikopo hiyo.”
Alibainisha, mikopo hiyo inatolewa ili kuwasaidia wananchi kupitia vikundi ili kuibua na kuendeleza miradi ya maendeleo ambayo itawanufaisha wao na wategemezi wao.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Simanjiro, Sendeu Laizer alimshukuru Mkurungenzi wa Halmashauri hiyo na baraza la madiwani  kwa kuhakikisha anatenga fedha hizo kwa kuwahudumia makundi maalumu.
Laizer aliishukuru benki ya NMB kwa kuwajengea  makundi hayo uwezo wa  elimu ya kifedha, jambo ambalo limesaidia kukopa na kuanzisha biashara zenye tija.
Mwisho


Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.