Na. Mwandishi Wetu, RUKWA
Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Red
Cross) kimeitikia wito uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
kwa kutoa Magodoro 100 na mablanketi 100 ili kuzisaidia kaya zaidi ya 300
zilizokosa mahala pa kulala baada ya nyumba zao kumezwa na maji ya ziwa
Tanganyika baada ya ziwa hilo kutapika na kuathiri vijiji vya Kasanga, Kilewani
na Kipwa vilivyopo Kata ya Kasanga, Wilayani Kalambo.
Hivi karibuni Mh. Wangabo aliziomba taasisi,
mashirika na wadau mbalimbali nchini kuona uwezekano wa kuzisadia kaya hizo ili
wananchi hao waweze kujihifadhi na mvua, baribdi pamoja na kuwapa misaada ya
kiafya kutokana na vyoo vya maeneo hayo kuchukuliwa na maji na hivyo kuwepo
uwezekano mkubwa wa magonjwa ya mlipuko kutokana na vinyesi kusambaa na hivyo
aliwataka wananchi hao kuchukua tahadhari za kiafya.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi akikabidhi mablanketi 100 na Magodoro 100 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mh. Julieth Binyura (kushoto) |
Wakati akipokea msaada huo kutoka Chama cha
Msalaba Mwekundu na kukabidhi kwa mkuu wa Wilaya ya kalambo kwa niaba ya Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Winnie Kijazi alifikisha
maelekezo ya Mkuu wa Mkoa kuwa wananchi waliopo katika maeneo hayo wanatakiwa
kuhama na hivyo kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kufanya haraka
kuwahamisha wananchi hao katika maeneo ambayo halmashauri imeyatenga.
“Wananchi Waelewe kwamba serikali inapotoa
misaada, basi ni kwaajili ya kuwasaidia wakati wa dharura, lakini kuendelea
kujiepusha kuishi kwenye maji kwasababu kwakweli ni hasara, serikali ina mambo
mengi ya kufanya, mmeona barabara zimejengwa vizuri, mmeona hospitali
zimejengwa vizuri, ni hela nyingi serikali inatumia kwahiyo wasikae wakategemea
kwamba serikali italeta na hii mwenyekiti (wa halmashauri) utusaidie kwenye
mikutano yako uwaelimishe wananchi watoke wkenye hayo ameneo,” Alisema.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh.
Julieth Binyura wakati akipokea msaada huo alikishukuru Chama cha Msalaba
Mwekundu kwa kuwapa msaada huo na kuwataka wananchi wa maeneo yaliyoathirika
kutoka kwenye maeneo hayo na kuanza kujenga katika maeneo yenye miinuko huku
akiwataka kujikinga na magonjwa ya kipindupindu pamoja na Corona.
“Nawaasa tu wananchi kwamba watakapokuwa
wamepata blanketi na magodoro, basi tunaomba kwasasa kwa vile mvua zimepungua
waanze kujenga maeneo ya mwinuko na tayari tumeshawaelekeza, Afisa Ardhi
ameshaelekeza, na vipimo wameshapewa wao ni kwenda kujenga kwenye mwinuko na
kuondoka kwenye ziwa ambapo tayari limeshajaa maji na mpaka sasa maji
yanaendelea kujaa bado halijapungua kwasababu kuna sehemu ambazo mvua bado
zinanyesha,” Alisisitiza.
Aidha, Mratibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu
Mkoani Rukwa Michael Mshingo aliwaomba wananchi wa Mkoa wa Rukwa kujiunga na
chama hicho ili kuweza kuongeza nguvu kazi ya chama hicho katika kutoa huduma
kwa jamii ndani ya mkoa na pia kuwaomba wananchi hao kuendelea kuchukua
tahadhari ya ugonjwa wa Corona kwa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni
pamoja na kuvaa barakoa.
Baadhi ya Wanachama wa Chama cha msalaba Mwekundu wakipakia magodoro na mablanketi katika lori kwaajili ya kupelekewa waathirika wa mafuriko ya maji ya ziwa Tanganyika Wilayani Kalambo |
Mbali na Chama cha Msalaba Mwekundu kutoa
Magodoro na Mablanketi yenye thamani ya Shilingi milioni 8 pia Mbunge wa jimbo
la Kalambo ambaye pia ni Naibu Waziri OR-TAMISEMI Mh. Josephat Kandege nae
ametoa turubai 50 pamoja na tani moja ya unga huku Mkuu wa mkoa akitoa turubai
16 na sukari kilo 100.
MWISHO
MWISHO
Comments
Post a Comment