Rais Magufuli Aagiza Wizara ya Fedha Kutoa Tsh. Bilioni 2 Ujenzi wa Ikulu Dodoma


Na. Jonas Kamaleki, DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa Shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kukamilishaujenzi wa Ofisi ya Ikulu, Chamwino, Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa Ofisi za Ikulu Chamwino Dodoma leo Mei 30, 2020
Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Ikulu, iliyofanyika leo Chamwino, Dodoma.
Akionyesha kuridhishwa na kazi inayofanywa na SUMA JKT Rais Magufuli amesema kuwa vijana 2400 wanoshiriki ujenzi huo atawafikiria ujenzi utakapokamilika.

Rais alisema kuwa kila kazi anayowapa JKT ana uhakika wanaifanya vizuri akitaja baadhi kama ujenzi wa ukuta wa Mirerani, mji wa Serikali, Dodoma na kushiriki katika misheni mbalimbali za kulinda amani ndani nan je ya nchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Marais wastaafu Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, Ali Hassan Mwinyi na Mama Maria Nyerere ambaye ni Mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa Ofisi za Ikulu ya Chamwino Dodoma leo Mei 30, 2020
“Kweli JKT mnastahili sifa mara 100 kutokana na kazi nzuri mnayofanya, hongereni sana”, alisema Rais Magufuli.

Aidha, amewapongeza watangulizi wake kwa hatua mbalimbali walizochukua kutimiza ndoto ya Baba wa Taifa ya kufanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi.

“Kwa kweli Nyerere aliona mbali, tangu nihamie Dodoma, nimepapenda sana, ni pazuri” alisisitiza Rais Magufuli na kuonyesha kuwa eneo la Chamwino lina mandhari ya kuvutia.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa pamoja na ujenzi unaoendelea, tayari majengo matatu ya awali na ujenzi wa ukuta unaozunguka Ikulu vimeshakamilika. Aidha, hakuna jengo hata moja la zamani litakalobomolewa.

Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya Pili, Mhe. Ali Hassan Mwinyi amemshukuru Rais Magufuli kwa uamzi wake wa kuhamishia Serikali Dodoma. Aidha, amemuelezea Rais Magufuli kuwa ni mchapakazi na mbunifu.

Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu amesema kuwa uamzi wa Serikali kuhamia Dodoma ni jitihada za muda mrefu na kila awamu ilifanya jitihada, Rais Magufuli amefanya mengi zaidi na sasa Serikali imehamia Dodoma.
Rais wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin Mkapa akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa Ofisi za Ikulu Chamwino Dodoma leo Mei 30,2020
Akitoa salamu kati hafla hiyo, Rais wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amempongeza Rais Magufuli kwa uamzi wa busara na wa hekima wa kujenga Ikulu, na kuongeza kuwa hapo ndio kilele chenyewe.

Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa Ofisi za Ikulu Chamwino Dodoma leo Mei 30,2020


Chanzo: Maelezo Blog

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.