Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKURUGENZI wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi
amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa
kuongoza mapambano ya virusi vya corona nchini na kuhamasisha wananchi kuchapa
kazi.
| Mkurugenzi wa Jiji, Godwin Kunambi |
Pongezi hizo alizitoa jana wakati akiongea na
waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri jana kuhusu
mkakati wa Halmashauri ya Jiji kuendelea kuwafundisha wanafunzi katika kipindi
cha mapumziko ya mapambano ya virusi vya corona.
Mkurugenzi kunambi alisema “ndugu waandishi wa habari
napenda kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya ya
kuongoza mapambano ya covid-19 nchini. Wakati huohuo, wakazi wa Jiji la Dodoma tuendelee
kuchukua tahadhari dhidi ya covid-19 kama tunavyoelekezwa na Wizara ya Afya kwa
sababu ugonjwa huo upo na ni hatari”. Aidha, alisema kuwa Halmashauri yake
itaendelea kutoa huduma za Afya na chakula kwa wagonjwa wa covid-19.
Katika mapambano hayo jijini hapa, aliupongeza uongozi
wa Hamlashauri chini ya Mshatiki Meya na Baraza la Madiwani kwa kazi nzuri
wanayofanya katika utoaji wa elimu ya kujikinga na virusi vya corona. “Katika mapambano haya tunafanya kazi vizuri na
kwa karibu na Mkuu wa Wilaya na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini” alisema
Kunambi.
Mkurugenzi Kunambi alisema kuwa kufuatia agizo la
serikali kufunga shule za msingi na sekondari nchini, wanafunzi wapo nyumbani.
“Halmashauri ya Jiji la Dodoma tunasema maisha lazima yaendelee na wanafunzi
wasome wakiwa nyumbani. Kipindi hiki wanafunzi wengi wapo nyumbani ila
changamoto kubwa ni uzururaji mtaani kwa sababu hawana kazi za kufanya
nyumbani. Tumekuja na jawabu la kuwafanya wasizurure kwa kuwaanzishia vipindi
katika redio zilizopo ndani ya Jiji la Dodoma” amesema Kunambi.
| Mkurugenzi wa Jiji (katikati) akielezea mikakati ya Jiji la Dodoma kufundisha wanafunzi |
Mkurugenzi huyo alizipongeza redio za Dodoma kwa
muitikio chanya wa kutoa vipindi kwa ajili ya kuwafundishia wanafunzi. “Ndugu
zangu hizi ni redio za mfano na za kizalendo kweli. Ushirikiano huu ni muhimu
kwa manufaa ya wanafunzi wa Jiji letu la Dodoma, na niwahakikishie
hatutawaangusha” alisisitiza Kunambi.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina
jumla ya shule za msingi 133 zenye jumla ya wanafunzi 113,441 na shule za Sekondari 56 zikiwa
na wanafunzi 30,785.
MWISHO
Comments
Post a Comment