MKURUGENZI KUNAMBI AFURAHIA UBUNIFU WA WAKUU WA IDARA ELIMU MSINGI NA SEKONDARI JIJI LA DODOMA


Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma yapongeza ubunifu wa wakuu wa Idara ya Elimu Msingi na Sekondari katika kuwafundisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kipindi hiki cha mapumziko ya mapambano ya virusi vya corona.
Mkurugenzi wa Jiji, Godwin Kunambi
Pongezi hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi wakati akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri jana kuhusu mkakati wa Halmashauri ya Jiji kuendelea kuwafundisha wanafunzi katika kipindi cha mapumziko.

Mkurugenzi Kunambi alisema “pongezi kwa wakuu wa Idara ya elimu msingi na sekondari wa Halmashauri ya Jiji kwa ubunifu huu wa kuwafundisha wanafunzi kupitia redio za Dodoma na mitandao kipindi hiki cha mapumziko ya mapambano ya virusi vya corona”. 

Halmashauri ya Jiji la Dodoma inazo shule za msingi 133 zenye jumla ya wanafunzi 113,441 na shule za sekondari 56 zenye wanafunzi 30,785, aliongeza. “Ndugu waandishi wa habari mtaona idadi hii kubwa ya wanafunzi wapo nyumbani. Changamoto kubwa ni uzururaji wa wanafunzi mitaani kwa sababu hawana kazi za kufanya nyumbani. Sasa tumekuja na jawabu la kuwafanya wasizurure. Tumewaadalia vipindi katika redio za Dodoma na mitandao ya kijamii” alisema Kunambi.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika kipindi hiki watajikita katika kufundisha madarasa yanayofanya mitihani ya kitaifa. Aliyataja madarasa hayo kwa elimu ya msingi kuwa ni darasa la nne na la saba na kwa elimu ya sekondari kidato cha pili na cha nne. “Napenda kuwapongeza walimu wote wa shule za msingi na sekondari waliojitolea kuandaa vipindi kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi kipindi hiki cha mapumziko. Kazi wanayofanya ni nzuri na heshima kubwa kwa Halmashauri yetu ya Jiji la Dodoma.  

Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Upendo Rwenyemamu alisema kuwa katika vipindi vitakavyofundishwa ni masomo yote kidato cha pili na cha nne. Walimu 26 wabobezi wameandaliwa na ratiba ya vipindi hivyo itawekwa katika tovuti ya Halmashauri, aliongeza.

Nae Afisa Elimu Msingi wa Jiji la Dodoma, Mwl. Joseph Mabeyo alisema kuwa walimu wameandaliwa vizuri na mada zipo tayari kwa ajili ya wanafunzi.

MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.