Makonda atoa msaada kwa wajane Mkoani Dar es salaam


DAR ES SALAAM.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda ametoa msaada wa Mabati yenye Thamani ya shilingi Milioni 476 kwaajili ya Kuezeka Nyumba 1,000 za Wajane mkoani humo ambao nyumba zao zimeathiriwa na mafuriko yanayotokana na Mvua zinazoendelea kunyesha ambapo amewataka Wananchi waliojenga mabondeni kuondoka.

RC Makonda amesema hayo wakati wa Ziara ya Kukagua athari za Mvua  na kubaini uwepo wa familia za Wajane ambao Nyumba zao zimechukuliwa na Mafuriko na sasa wanapitia changamoto ya kuhifadhiwa kwa majirani baada ya kukosa makazi ya kuishi hivyo ameona ni busara kutoa msaada huo kama sehemu ya pole kwa adha waliyoipata.

Aidha RC Makonda amewapa siku 10 Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanapitia maeneo ya Mito na Mabonde kukagua athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwashirikisha viongozi wa mitaa ili kwa pamoja watoe mapendekezo ya nini kifanyike kisha wampatie ripoti ya kuonyesha hatua za kukabiliana na Mafuriko ya Mara kwa Mara.

Aidha RC Makonda amesema athari zinazoonekana kwa sasa ni matokeo ya Jamii kuwafumbia macho watu wanovunja sheria kwa kujenga mabondeni, kuchimba mchanga na kuziba mikondo ya maji jambo linalopelekea Mafuriko hivyo ametaka kila mwananchi kuwa mlinzi wa mwenzake.

Pamoja na hayo RC Makonda amesema kwa sasa serikali inaendelea kurejesha miundombinu na madaraja yaliyochukuliwa na Mafuriko ikiwemo ujenzi wa madaraja ya muda mfupi ili kuwezesha shughuli za kijamii kuendelea.

RC Makonda pia amewaelekeza wakandarasi kutumia kipindi hiki cha mvua kuangalia kama Design ya madaraja wanayojenga yanakidhi kuhimili na kupitisha maji ya mvua ili wabuni design mpya zinazokidhi viwango.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.