KUSAYA: VIJANA JIFUNZENI KILIMO BIASHARA


Na. Revocatus Kassimba, MOROGORO
Vijana wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini wameshauriwa kujitokeza na kupata mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo biashara kwa ajili ya kujipatia ujuzi na ajira toka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya akikagua kitalu nyumba kilichopandwa nyanya na vijana walliopo katika Kituo Atamizi cha Vijana kujifunza Kilimobiashara chini ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine mjini Morogoro
Wito huo umetolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya wakati akiongea na vijana wanaondelea na mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo biashara katika Kituo Atamizi cha Vijana cha Kilimobiashara (SUA-AIC Youth Agribusiness Incubators) mjini Morogoro.

“Vijana tunatambua uwepo wenu hapa kituoni,jitahidini kujifunza mbinu bora za kilimo mkilenga kujiajili  na mwisho wa mafunzo yenu mrudi vijijini na mijini kuwa walimu kwa vijana wenzenu” alisema Kusaya.

Katibu Mkuu Kusaya aliwapongeza vijana hao kwa kuamua kujiunga na kambi atamizi kwani wanatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwataka vijana kujiajili kupitia kilimo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya akiwa ameshika hoho za rangi zinazozalishwa na vijana katika kituoo atamizi cha mafunzo kwa vitendo chini ya SUA.Kulia kwake ni Msimamizi wa kituo hicho Zebedayo Sanga na kushoto kwake ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine, Prof. Raphael Chibunda
“Lengo la serikali ya Awamu ya Tano ni kukifanya kilimo kuwa ni ajira na kazi inayochangia kukuza uchumi wa nchi,ndio maana nimekuja kuwatembelea na kuwatia moyo “ alisisitiza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo.

Akitoa taarifa ya kituo hicho,Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Prof. Raphael Chibunda alisema kituo atamizi kinafundisha vijana wahitimu wa vyuo mbalimbali wanaopenda kufanya kilimo biashara.

Alisema kwa sasa kuna vijana wapatao 40 wanaoendelea na mafunzo kwa vitendo kwa mwaka mmoja wakizalisha mazao ya mboga mboga kama hoho za rangi,matango na nyanya kwa usimamizi wa wataalam wa chuo.
Sehemu ya vijana wanaopata mafunzo kwa vitendo katika kituo atamizi  Chuo Kikuu cha Sokoine kujifunza kilimobiashara wakimsikiliza Katibu Mkuu wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya (hayupo pichani) wakati alipowatembelea hivi karibuni mjini Morogoro
Akielezea manufaa ya kituo hicho Hefsiba Olloo kutoka Kilimanjaro alisema ameweza kuzalisha nyanya kwenye kitalu nyumba na kuvuna kilo 1,318 za nyanya zilizompatia shilingi milioni 4 ndani ya kipindi cha miezi minne.

Mafanikio aliyopata mwaka huu Januari alivuna kilo (338) Februari (400),Machi (400) na Aprili amevuna (180) ambazo ameuza kwa bei ya shilingi 2500 hadi 3000 kwa kilo moja.

 “Kwa muda mfupi tangu nimejiunga na kambi atamizi hapa SUA mwezi Septemba 2019 tayari nimeona manufaa yake kwa kuwa na uhakika wa kipato kupitia kilimo cha nyanya .Nilipanda nyanya mwezi Octoba mwaka 2019 na sasa naendelea kuvuna” alisema Hefsida.

Hefsida alihitimu shahada ya Sayansi  katika Hisabati (Bachelor of Science in Mathematics) Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2018 na hakuweza kupata ajira hivyo akaamua kuanzisha kilimo cha mboga.

Kwa upande wake msimamizi wa kituo atamizi Zebedayo Sanga ambaye ni mhitimu wa digrii ya Horticulture mwaka 2018 toka SUA aliwahamasisha vijana wengi zaidi waliopo mitaani kuja kujifunza kilimobiashara na kuwa na uhakika wa kipato na ajira.

Mwisho

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.