CD KUNAMBI AWATAKA WAZAZI KUSIMAMIA WANAFUNZI KUSOMA KUPITIA REDIO


Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAZAZI katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kuwasimamia wanafunzi ili waweze kujisomea kupitia vipindi vinavyoendelea katika redio zilizopo jijini hapa ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Mkurugenzi wa Jiji, Godwin Kunambi akisisitiza jambo
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi wakati akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri jana kuhusu mkakati wa Halmashauri ya Jiji kuendelea kuwafundisha wanafunzi katika kipindi cha mapumziko ya mapambano ya virusi vya corona.

Mkurugenzi Kunambi alisema kuwa urithi mkubwa kwa watoto ni elimu na si mali kama baadhi ya watu wanavyofikiria. “Nichukue nafasi hii kuwaomba wazazi na walezi kuhakikisha Watoto wao ambao ni wanafunzi wanatimiza wajibu wao kwa kujisomea kupitia vipindi tunavyoendelea navyo vya redio na mitandao mbalimbali ya kijamii. Hakikisheni mnatembelea tovuti ya Jiji ambayo ni www.dodomacc.go.tz kwa ajili ya kujifunza” alisema Kunambi.

Wakati huohuo, Mkurugenzi huyo aliwashauri wazazi na walezi ambao hawana redio kununua redio ili watoto wapate fursa ya kujifunza kupitia vipindi vya redio.  

Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl Upendo Rwenyemamu amesema kuwa katika vipindi vitakavyofundishwa ni masomo yote kidato cha pili na cha nne. Walimu 26 wabobezi wameandaliwa na ratiba ya vipindi hivyo itawekwa katika tovuti ya Halmashauri, aliongeza.

Nae Afisa Elimu Msingi wa Jiji la Dodoma, Mwl Joseph Mabeyo alisema kuwa katika darasa la nne masomo sita yatafundishwa. Kwa wanafunzi wa darasa la saba, masomo yatakayofundishwa ni matano. Walimu wameandaliwa vizuri na mada zipo tayari kwa ajili ya wanafunzi” amesema Mwl Mabeyo kwa kujiamini.

MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.