BODI YA MKONGE YATEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU


Na. Revocatus Kassimba, TANGA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya ameipongeza Menejimenti ya Bodi ya Mkonge na watumishi kwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu la kuhamia katika ofisi iliyotwaliwa na serikali hivi karibuni kutoka kwa wamiliki binafsi.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Martin Shigela (katikati) akiongoza mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo kuhusu mkakati wa kuinua zao la mkonge mkoa wa Tanga

Kusaya ametoa pongezi hizo jana Jijini Tanga wakati alipokwenda kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu mwezi Machi mwaka huu kufuatia ripoti ya kamati ya uchunguzi kuhusu mali za bodi ya mkonge kumilikishwa kwa watu binasfi kinyume cha utaratibu.

“Nawapongeza menejimenti mpya ya Bodi ya Mkonge kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kuhamia katika jengo hili na kuendelea na kazi za kusimamia zao la mkonge”alisema Kusaya.

Waziri Mkuu aliagiza kuwa jengo lililokuwa linamilikiwa visivyo halali na Willian Kimweli Madundo na kulitumia kama Medicare hospital Tanga litumike kuwa makao makuu ya bodi kwani miaka ya nyuma ndipo palikuwa makao makuu ya Mamlaka ya Mkonge Tanzania.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald  Kusaya  (aliyevaa tai) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao Bw.Nyasebwa Enock kuhusu bodi ya mazao kuweka bango la ofisi eneo hilo. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Saad Kambona
Aidha, Katibu Mkuu huyo aliigiza bodi ya mkonge kuhakikisha inafuatilia mali zake ikiwemo nyumba 32 ambazo zilirejeshwa serikalini “nataka waliokuwa wamiliki wapewe notisi na kuondoka au wapewe mikataba ya upangaji haraka” alisisitiza.

“Bado kuna nyumba mbili nchini Uingereza,nataka zirejeshwe serikalini na zile nyumba mbili jirani na Mkonge hotel hapa Tanga zifuatiliwe kujua uhalali wa umiliki wake “ alisema Katibu Mkuu huyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Saad Kambona alimweleza Katibu Mkuu kuwa tayari wameanza kufanya kazi kwenye jengo jipya la ofisi kama walivyoagizwa na wamefanya ukarabati mdogo kuwezesha jengo hilo kutumika kama ofisi badala ya ofisi za zamani uwanja wa gofu Tanga.

Kambona alisema kwa sasa wanaiomba serikali kuendelea kuiwezesha bodi ili iweze kuhudumia zao la mkonge wakati ikijipanga kuanza kujitegemea kimapato.
Picha ya pamoja kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya ( aliyevaa tai) na Menejimenti ya Bodi ya Mkonge mara baada ya kukagua jengo la ofisi kufuatia agizo la Waziri  Mkuu la kuitaka bodi ihamie hapo toka ofisi za zamani uwanja wa gofu jijini Tanga. Jengo hilo awali lilifahamika kama Medicare Hospital Tanga
"Tuna lengo baada ya kuimarisha usimamizi wa zao la mkonge nchini,bodi iweze kutoa gawio kwa serikali “alisema Kambona.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela aliipongeza Wizara ya Kilimo kwa jitihada zake za kufufua zao la mkonge kwani ndio uti wa mgongo wawananchi wa Tanga.

Shigela alisema ni wakati sasa wizara ya kilimo ikaongeza msukumo katika kuhakikisha mbegu za mkonge zinapatikana kwa wingi na wakulima wanazipata kwa gharama nafuu.

Mwisho

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.