SIMAMIENI MIRADI KWA KUZINGATIA MATUMIZI YA VIFAA KATIKA VIWANGO VILIVYOELEKEZWA NA SERIKALI-MWAMBAMBALE
Na Mwandishi wetu, Kilosa
Wito umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kilosa Asajile Mwambambale kwa wasimamizi mbalimbali wa miradi na kamati za
ujenzi katika kata na vijiji kuhakikisha shughuli zote za ujenzi zinazingatia
maelekezo ya viwango vya vifaa vilivyoelekezwa na Serikali.
Mwambambale ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya ukaguzi
wa miradi akiwa ameambatana na timu ya menejimenti ya Halmashauri ambapo
amesema kuwa vifaa hivyo vinapaswa kukidhi mahitaji na viwango vilivyoelekezwa
na Serikali ili kupata matokeo mazuri ya miradi hiyo ili iweze kudumu kwa
muda mrefu na kutumika na vizazi vijavyo.
Akiwa ameambatana na timu ya menejimenti katika kituo cha afya
Malolo ameelekeza kuwa wakati wa kiangazi nguvu kazi ya wananchi ianze
kuandaa matofari kwa ajili ya wodi tatu kwa maana ya wodi ya wanaume, wanawake
na watoto sambamba na jengo la kuhifadhia maiti, huku akisema kuwa ni matumaini
yake kuwa kituo cha Malolo kitakapokamilika kitatoa huduma zote za msingi ili
kuwaondolea wananchi adha ya kwenda umbali mrefu kupata huduma huku akisema
kituo hicho kitahudumia wananchi wengi toka maeneo mbalimbali.
Aidha amesema kuwa anatarajia kuanzia mwezi Julai kituo hicho
kitakuwa kimefanya maandalizi ya kutosha na kwamba ofisi ya Mkurugenzi
inategemea kuanza kupokea mahitaji ya uwezeshwaji wa vifaa na ufundi kwa ajili
ya wodi hizo na kwamba kama Wilaya ingependa ujenzi katika kituo hicho
kukamilika kwa wakati ili huduma zianze kutolewa mara moja kwa wananchi ambapo
kituo hicho kinatarajiwa kukamilika mwezi Mei na kwamba kituo cha afya Malolo
ni kituo cha mfano kwani kimejengwa na wananchi wenyewe.
Akijibu changamoto zilitolewa za uhaba wa watumishi wa idara ya
elimu na kilimo Mkurugenzi amesema litafanyiwa kazi huku akiitaka idara ya Kilimo
kufanyia kazi changamoto ya ugonjwa wa zao la vitunguu, sambamba na hayo
ameahidi kuchimbwa kwa kisima kirefu katika kata ya Malolo kazi itakayofanywa
na Halmashauri ili kutatua changamoto ya uhaba wa maji ambayo wananchi wamekuwa
wakitumia maji ya mtoni ambayo yamekuwa yakisababisha ugonjwa wa kichocho.
Kwa upande wa kituo cha afya Mikumi ambacho ujenzi wa wodi mbili
za wanawake na wanaume unaendelea amesema kwa siku za baadaye kinatarajiwa
kiweze kupata hadhi ya kuwa sawa na hospitali ili kiweze kuhudmuia
wanacnhi wengi kwa kadri inavyowezekana kwani huduma za mahali hapo zinalenga
zaidi kuhudumia wananchi kwa bei nafuu lakini pia ametaka ujenzi wa wodi hizo
kasi iongezwe ili ifikapo mwezi Aprili wodi hizo ziwe zimekamilika ambapo
ujenzi huo unafadhiliwa na fedha za Serikali una unatarajiwa kutumia shilingi
milioni 140 na kwasasa uko katika hatua za upauaji.
Nao wananchi wa kata za Malolo na Mikumi wameshukuru kwa ujenzi
unaondelea katika maeneo yao kwani kabla ya kuwepo kwa vituo hivyo walikuwa katika
adha kubwa ya kutafuta huduma katika maeneo ya jirani ambapo walikuwa wakitumia
gharama kubwa ili kupata huduma lakini pia kutembea umbali mrefu jambo
linalowagharimu fedha na muda lakini kwa sasa wanashukuru kwani adha hizo
zimeanza kutoweka na kwamba wanatarajia huduma zote za msingi zitakapotolewa
katika vituo hivyo zitakuwa zimewapunguzia gharama mbalimbali kama za matibabu
na usafiri.
Comments
Post a Comment