Na. Amiri Kilagalila, NJOMBE
Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Njombe (CCM), Neema
Mgaya amesema ili elimu iendelee kukua hapa nchini ni lazima shule
mbalimbali zianze kutumia vifaa vya kisasa katika kufundishia kama mbinu
mbadala ili wanafunzi waweze kufanya vizuri katika masomo yao kulingana na
teknolojia inavyokua kwa kasi duniani.
Amezungumza hayo alipokuwa katika ziara ya kutembelea shule ya
sekondari Maria Nyerere ambayo ina mradi wa madarasa matatu yanayogharimu
milioni 60, pamoja na shule ya sekondari Wanging'ombe na Ludewa sekondari ambapo
amegawa jumla ya tarakilishi (kompyuta)10, vichapishi (Printer) 2, huku akiahidi
kufunga mfumo wa interneti katika shule hizo.
Baadhi ya wakuu wa shule zilizonufaika na misaada hiyo
akiwemo mwalimu Optatus Mng'ong'o mkuu wa shule ya sekondari Wanging'ombe
pamoja na Paulo Mtunduru mkuu wa shule ya sekondari Ludewa,wanasema kuwa misada
hiyo itasaidia kuongeza ujuzi kwa walimu kwani watakuwa na fursa kubwa ya
kujisomea kupitia mitandao baada ya uwepo wa computer katika shule zao.
Afisa elimu Wilaya ya Ludewa, mwalimu Matenus Ndumbalo pamoja na
afisa elimu sekondari Wilaya ya Wanging'ombe, Joyce Mgonja wameshiriki
makabidhiano hayo ambapo wamesema kuwa kulingana na teknolojia inavyokua kwa
kasi hivi sasa ni lazima matumizi ya Kompyuta yaongezeke mashuleni ili kutanua
uelewa kwa wanafunzi pamoja na walimu na hivyo kusidia kukuza kiwango cha elimu
hapa nchini.
MWISHO
Comments
Post a Comment