OFISI YA ARDHI MARA KUWEZESHWA VIFAA VYA UPIMAJI



Na Munir Shemweta, WANMM MUSOMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema wizara yake itaipatia ofisi ya ardhi mkoa wa Mara vifaa vya upimaji ili viweze kutumiwa na halmashauri za mkoa huo  kwa lengo la kuongeza kasi ya upimaji.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana wilayani Musoma mkoa wa Mara alipokwenda kukagua ofisi mpya ya ardhi ya mkoa Mara ikiwa ni jitihada za wizara ya ardhi kusogeza huduma za ardhi kwa wananchi.
Awali huduma za ardhi zilikuwa zikitolewa na ofisi za Mkamishna Wasaidizi wa Kanda ambapo kanda moja ilikuwa ikihudumia zaidi ya mikoa miwili jambo lililokuwa likiwapa usumbufu wamiliki wa ardhi kwenda umbali mrefu kuifuata huduma hiyo.

Alisema, baada ya wizara yake kuanzisha ofisi za mikao sasa wananchi watapata huduma za ardhi katika mikoa husika na migogoro ya ardhi sasa itapatiwa ufumbuzi kupitia wataalamu watakaokuwa katika mikoa hiyo.

Alibainisha kuwa, katika jitihada za kuongeza kasi ya upimaji maeneo mbalimbali ofisi za mikoa zitapatiwa vifaa vya upimaji ili visaidie halmashauri kupanga, kupima na kumilikisha ardhi na kusisitiza vifaa hivyo vitatolewa bure na aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana na ofisi za ardhi za mikoa.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula, Wizara yake imeamua kubeba jukumu la kutoa vifaa vya upimaji ili kuongeza kasi ya upimaji ingawa jukumu hilio linapaswa kufanywa na halmashauri kwa kuwa ndizo zenye mamlaka za upangaji miji katika maeneo.

Dkt Mabula amesikitishwa na kiasi kidogo kinachotengwa na halmashauri kwa ajili ya kazi za kupanga, kupima na kumilikisha ardhi ambapo alitolea mfano wa halmasahauri ya Musoma kutenga milioni 30 kwa kazi mbalimbali za sekta ya kiasi alichokieleza kuwa  kidogo.

‘’Milioni 10 au 15 utapima viwanja vingapi? Halmashauri hazijaipa kipaumbele sekta ya ardhi ndiyo maana malalamiko yanakuwa mengi, muongeze bajeti za upimaji’’ alisema Dkt Mabula

Hata hivyo, ameishauri halmashauri ya wilaya ya Musoma kuwatumia wataalamu wake kwa kuandika andiko ili kupatiwa mkopo usio na riba unaotokewa na wizara kwa ajili ya shughuli za umilikishaji ardhi ambapo alisema katika kipindi caha bajeti ijayo wizara inatarajia kupata bilioni saba kwa ajili ya kuzikopesha almashauri.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt Vincent Naano Anney aliipongeza wizara ya ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa uamuzi wake wa kuanzisha ofisi za mikoa na kueleza kuwa uamuzi huo utaleta  nafuu kwa wananchi wa mara katika kupata huduma za ardjhi ambapo awali iliwalazimu kusagiri hadi Simuiyu kupata huduma  hiyo.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.