NHC YATAKIWA KUKAMILISHA UJENZI JENGO LA KITEGA UCHUMI MUTUKULA


Na. Munir Shemweta, WANMM MISENYI


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukamilisha haraka mradi wake wa ujenzi wa Jengo la Kitega Uchumi lililopo mpaka wa Tanzania na Uganda eneo la Mutukula wilaya ya Misenyi mkoani Kagera ili kuliwezesha shirika kupata faida kupitia jengo hilo.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula (Kulia)

Dkt. Mabula alitoa agizo hilo juzi wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo akiwa katika ziara yake mkoani Kagera kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo sambamba na kufuatilia utekelezaji maagizo aliyoyatoa kuhusiana na wa sekta ya ardhi.

Alisema, mradi wa jengo la kitega uchumi unaoendelea eneo la Mutukula uko sehemu nzuri ya mpakani mwa Tanzania na Uganda na kuna muingiliano mkubwa wa kibiashara hivyo ni vizuri Shirika la Nyumba likaona haja ya kuharakisha ujenzi wake ili kutoa fursa kwa taasisi na wawekezaji kupanga kwenye jengo hilo.

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, mji wa Mutukula umechangamka na una mzunguko mzuri wa biashara hatua inayosababisha kuwepo mvuto kwa wafanyabiashara na wawekezaji katika eneo hilo na kukamilika kwake kutaiwezesha NHC   kupata wapangaji na kujipatia mapato.
“Naagiza Miradi yote ya Shirika la Nyumba la Taifa inayoweza kuliingizia Shirika mapato likiwemo hili la kimkakati lazima iishe ili NHC iingize mapato na kujiendesha kibiashara’’ alisema Dkt. Mabula.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mikoa ya Kagera na Geita, Benit Masika alisema shirika lake liko katika jitihada kubwa za kuhakikisha mradi huo wa jengo la kitega uchumi Mtukula unakamilika mapema na kubainisha kuwa kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 88 na utakapokamilika litapangishwa kwa taasisi zilizoonesha nia ya kupanga zikiwemo za kifedha kama vile mabenki.

Aidha, Nabu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliitaka Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera kutumia vizuri fursa ya kuwa eneo la mpakani kwa kuhakikisha inakamilisha zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha viwanja ili wananchi waweze kujenga nyumba nzuri na zenye sura ya nchi ya Tanzania.

Alisema, Halmashauri ya Misenyi wakati wa kupanga mji huo ihakikishe inakuwa na soko la mazao zikiwemo ndizi ili kuwawezesha watanzania kuuza bidhaa zao nchini Uganda tofauti na sasa ambapo tegemeo kubwa lipo upande wa Uganda na kuwataka watanzania kubadilika kwa kuitumia fursa ya kuwa eneo la mpakani kuchangamkia kuwekeza katika ardhi.

MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.