NAIBU WAZIRI MABULA ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA MARA




Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi wa Ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Mkoa wa Mara Injia Kazoba Wilson (kushoto) wakati akitoka kukagua maendelezo ya ujenzi wa hospitali hiyo jana Musoma mkoani Mara. Wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt Vincent Naano Anney.



Na Munir Shemweta, WANMM, MUSOMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara iliyoko Kwangwa Musoma unaogharimu takriban Bilioni 15.082.

Dkt Mabula aliridhishwa na kasi ya mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo alipokwenda kukagua maendeleo ya ujezi wake jana wakati akiwa katika ziara ya siku moja mkoani Mara.

Alisema, ujenzi wa mradi huo ni ukombozi kwa wananchi wa Mara sambamba na mikoa na nchi jirani kwa kuwa itakuwa ikitoa huduma za kitabibu kwa wananchi wa maeneo hayo.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alibainisha kuwa, hana mashaka na Shirika la Nyumba la Taifa katika kutekeleza mradi huo kutokana na Shirika hilo kufanya vizuri kwenye miradi mbalimbali inayosimamia.

‘’Kwa sasa sina mashaka na Shirika la Nyumba la Taifa katika masuala ya ujenzi kutokana na kufanya vizuri kwenye miradi mingi ya ujenzi inayosimamia lakini kinachotakiwa hapa ni kukamilisha ujenzi kwa wakati’’ alisema Dkt Mabula

Ameitaja baadhi ya miradi ya ujenzi inayofanywa na NHC na kufanya vizuri kwenye maeneo mablimbali kuwa ni ujenzi wa ofisi kumi na saba za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),  Hospitali ya Rufaa ya Kusini iliyopo Mtwara, Ofisi ya wilaya ya Wang’ingombe na nyumba za wakuu wa wilaya za Hai na Ulanga.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mara Goodluck Thomas alisema Shirika lake katika kutekeleza mradi huo tayari baadhi ya kazi zimekamilishwa ikiwemo jengo la Huduma ya Mama na Mtoto, nyongeza ya ghorofa moja na kupaua, kupiga plaster nje na ndani, maandalizi ya rangi, fremu za milango pamoja na kuweka marumaru.

Kwa mujibu wa Goodluck, kazi zinazoendelea sasa ni uwekaji mifumo ya maji safi na maji taka, kazi ya umeme, uwekaji mifumo ya gesi, ufungaji madirisha ya alminiuam na ukamilishaji kazi nyingine ukiendelea na mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo umefikia asilimia 65.

Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt Vincent Naano Anney alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa wakati ujenzi wa hospitali hiyo ukiendelea kukamilishwa kuna haja kwa mamlaka husika  kuanza kuangalia mahitaji ya Wataalamu na Vifaa vinavyohitajika kwenye vitengo mbalimbali vya hospitali hiyo na kubainisha kuwa kazi hiyo isipofanyika mapema kuna hatari ujenzi utakapokamilika hospitali hiyo ikakosa wataalamu wa kutosha kutokana na ukubwa wake.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.