Na. Gladys Gabriel, KILOSA
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kilosa, Asajile Mwambambale amewataka wasimamizi wa miradi na kamati za ujenzi
katika kata na vijiji kuhakikisha shughuli zote za ujenzi zinazingatia viwango na
vya vifaa vinavyotumika katika ujenzi ni vile vilivyoelekezwa na Serikali.
Maelekezo hayo ameyatoa leo katika ziara yake ya ukaguzi
wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.
Mkurugenzi Mwambambale amesema kuwa vifaa vinavyotumika
katika ujenzi vinapaswa kukidhi mahitaji na viwango vilivyoelekezwa na Serikali
ili kupata matokeo mazuri ya miradi hiyo. Kufuata maelekezo hayo kutaifanya
miradi inayojengwa kudumu kwa muda mrefu na kutumika na vizazi vijavyo,
aliongeza.
Katika Kituo cha Afya Malolo, Mkurugenzi huyo ameelekeza
kuwa wakati wa kiangazi nguvu kazi ya wananchi ianze kuandaa matofari kwa ajili
ya wodi tatu za kituo hicho. Alizitaja wodi hizo kuwa ni wodi ya wanaume, wodi
ya wanawake na watoto sambamba na jengo la kuhifadhia maiti.
Alisema kuwa kituo hicho cha Afya kitakapokamilika
kitatoa huduma zote za msingi ili kuwaondolea wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu
kupata huduma za afya wilayani humo. Kituo hicho kitahudumia kitahudumia
wananchi wengi toka maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo, alisisitiza.
Aidha, amesema kuwa anatarajia kuanzia mwezi Julai
kituo hicho kitakuwa kimefanya maandalizi ya kutosha na ofisi yake inategemea
kuanza kupokea mahitaji ya uwezeshwaji wa vifaa na ufundi kwa ajili ya wodi hizo.
Ameongeza kuwa matarajio ya Wilaya ujenzi wa kituo hicho kukamilika kwa wakati
ili huduma zianze kutolewa mapema kwa wananchi. Mkurugenzi amekitaja kituo
hicho kuwa cha mfano kutokana na kujengwa na wananchi wenyewe.
Katika kituo cha Afya Mikumi ambapo ujenzi wa wodi
mbili za wanawake na wanaume unaendelea Mkurugenzi Mwambambale amesema kwa siku
za baadaye kinatarajiwa kiweze kupata hadhi ya kuwa sawa na hospitali. Kupanda
hadhi kituo hicho kutawezesha kupanua wigo wa uhoaji huduma na kiweza kuhudumia
wananchi wengi kwa kadri inavyowezekana, aliongeza kwa gharama nafuu.
Wakati huohuo, ameagiza ujenzi wa wodi hizo uongezwe
kasi ili ifikapo mwezi Aprili ziwe zimekamilika. Ujenzi huo unafadhiliwa na
fedha za Serikali ukitarajiwa kutumia shilingi milioni 140, ukiwa katika katika
hatua za upauaji.
Nao wananchi wa kata za Malolo na Mikumi
wameshukuru kwa ujenzi unaoendelea katika maeneo yao kutokana na adha kubwa ya
kutafuta huduma za afya katika maeneo ya mbali kwa gharama kubwa.
Katika ziara hiyo ya kutembelea miradi ya
maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mkurugenzi
huyo aliambatana na timu ya menejimenti ya Halmashauri hiyo (CMT).
MWISHO
Comments
Post a Comment